Mahakama ya Wilaya ya Bukoba imemhukumu kijana mmoja Emaya Cleophas (20) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kumuoa mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya Sekondari Kabugalo iliyoko wilayani Bukoba.
Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Bukoba, Joseph Luambano amemtia hatiani kijana huyo kwa mujibu wa sheria ya elimu inayoelekeza kuwa kwa yeyote anayepatikana na kosa kama hilo atahukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Wakili wa Serikali Haruna Shomaje ameeleza kuwa katika mkoa wa Kagera na katika Mahakama hiyo ya Wilaya ya Bukoba, kesi ya aina hiyo imekuwa ni ya kwanza na kutoa angalizo kwa wakazi wote wa Mkoa wa Bukoba kutojaribu kujihusisha kimapenzi na wanafunzi kwani sheria itachukua mkondo wake.
“Hii ni kesi ya kwanza katika Mahakama hii iliyoamriwa namna hiyo na tunatoa angalizo zaidi kwa wakazi wa Bukoba Mjini, Wilaya nyingine mbalimbali na vitongoji vyote vya Mkoa wa Kagera kwamba sheria kali iko hivi. Wasijaribu hata kidogo, hata kuthubutu, hata kuwasogelea kabisa wanafunzi kwa sababu adhabu yake ni kali,” amesema Wakili Haruna Shomaje.
Wakili Haruna ameeleza kuwa jamii bado haijatambua kama ni kosa kuwaozesha wanafunzi kwani katika kesi hii familia za pande zote mbili (binti na kijana) ziliridhia kufungwa kwa ndoa hiyo, huku akiwataka wananchi wote kuitambua sheria hiyo ili wasijikute wakiingia hatiani pasipo kutambua.
“Changamoto kwa kesi hii ni kwamba inavyoonekana ni kwamba wananchi wengi bado hawajajua kama ni kosa kuozesha wanafunzi. Na inaonekana kwenye kesi hii upande wa binti walisema kwamba wameridhia binti yao kuolewa na hata upande wa mwanaume pia walisema kwamba binti huyo aliridhia kuolewa. kwa hiyo inaonekana kwamba elimu kuhusu suala la sheria hii bado iko chini na sisi tunasema kwamba kupitia kesi hii ni vyema watu wote wakajua kwamba sheria iko hivi na inabana pande zote mbili,” Amesema Haruna.