Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo amewataka wananchi kumuunga mkono Rais John Magufuli katika kufufua uchumi.
Akihubiri wakati wa ibada ya mkesha wa Krismasi jana Jumapili Desemba 24,2017 katika Kanisa la Mtakatifu Maurus lililopo Kurasini, Kardinali Pengo amesema wananchi wamuunge mkono Rais kwa kufanya kazi badala ya kuwa walalamikaji.
"Magufuli na wasaidizi wake tuwaunge mkono kwa kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo," amesema.
Kardinali Pengo amesema watu wanapofanya kazi kwa bidii nchi inakuwa na amani ambayo ndiyo msingi wa maendeleo.
"Wakati umefika wa watu kufanya kazi usiku na mchana, hilo likifanyika nchi itaendelea kuwa na amani. Muda wote uwe wa kufanya kazi bila kujali ni usiku au mchana, tupumzike kidogo kwa ajili ya kupata usingizi," amesema.
Kardinali Pengo amesema amani ya kweli duniani haitokani na viongozi waliopo madarakani bali wananchi wenyewe.
Amesema kila mtu afahamu kwamba chimbuko la amani ni kufanya kazi halali inayopendeza machoni mwa Mungu.
Amewataka wananchi kuliombea Taifa na viongozi wake ili waendelee kusimamia ujenzi wake.