SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 4 Desemba 2017

T media news

Familia Yaeleza Nyuma ya Pazia Shambulio la Lissu


FAMILIA ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, imesema kuwa watoto wake wanapitia wakati mgumu kwa kuwa tukio la kupigwa risasi kwa baba yao liliwaumiza kisaikolojia.

Aidha, watoto hao kwa sasa wanalazimika kuishi mbali na wazazi baada ya wazazi wote wawili kuwa nje ya nchi tangu Septemba 7, mwaka huu Lissu aliposhambuliwa kwa risasi 32 nje ya nyumba yake Area D, Dodoma.

Wakati Lissu akiwa amelazwa katika Hospitali ya Nairobi ambako amefanyiwa operesheni kadhaa tangu hapo kutibu majeraha ya risasi tano zilizompata mwanasiasa huyo, mkewe Alice anamuuguza.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, mdogo wa Lissu, Vicent Mughwai, alisema hiki ni kipindi kigumu sana kwa watoto wa mwanasiasa huyo.

Mbunge huyo kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amelazwa kwa siku 87 jijini Nairobi mpaka jana.

“Kwa ujumla ni kipindi kigumu sana kwa watoto, licha ya kwamba ni wakubwa wanasoma sekondari na walishakwenda kumuona baba yao, lakini wazazi wanapokuwa hawapo wote kwa muda wote huwa ni ngumu sana,” alifafanua Mughwai.

“Wanapitia kipindi kigumu, lakini kwa uwezo wa Mungu wanasonga mbele.

"Waliomuumiza Lissu wasifikiri wamemuumiza peke yake bali (na) watoto ambao walipenda kuwaona wazazi wao kama watoto wengine.

"Kwa ujumla ni kipindi kigumu sana (kwao).”

Mughwai alisema kwa kawaida watoto wangependa kuwaona wazazi wao, lakini hawapati nafasi hiyo jambo ambalo linawaathiri kisaikolojia.

Kwa mujibu wa mdogo wake huyo, mbali na kupelekea shida kwa watoto, watu waliompiga risasi Lissu pia walimuonea kwa kuwa "hakufanya jambo lolote baya".

Lissu alisimama kusema ukweli kwa manufaa ya Watanzania wa kizazi cha sasa na kijacho, alisema  Mughwai na kwamba watu hao wakachukulia kuwa uadui.

“Tunashukuru Mungu watoto hawajambo, wamefunga shule na wanaendelea na maisha yao," alisema Mughwai."Uzuri ni wakubwa, wanatambua na wanajisimamia vizuri.

"Imani yetu (kama familia) ni kuwa Lissu atarejea akiwa anatembea na kuendelea na majukumu yake kama kawaida.”Jumanne iliyopita Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu alimtembelea Lissu kumpa pole na kumfariji hospitalini hapo ambapo Mwanasheria Mkuu huyo wa Chadema alielezea kufurahishwa kwake na ujio huo na kuagiza salamu za shukrani kwa Rais John Magufuli.

ATASIMAMA, ATATEMBEAAidha, Mughwai alisema uhakika walionao kama familia ni kuwa siku chache zijazo Lissu atakwenda nje ya Kenya kwa matibabu zaidi na mazoezi na kwamba hadi sasa wanaridhishwa na hali ya ndugu yao.

"Yote ni Mungu tu ambaye amesimamia kila jambo linakwenda vizuri," alisema Mughwai. "Tunahakika kwa uwezo wake ndugu yetu atasimama, atatembea na kuendelea na shughuli zake kama kawaida."

Katika hatua nyingine, familia hiyo imedai kusikitishwa na Bunge kushindwa kumlipa Lissu nusu posho ya siku na asilimia 20 ya posho yake inayopaswa kulipwa kwa mtu anayemuhudumia hospitalini.

"Lissu ameumia akiwa kazini, lakini hadi tunavyozungumza hajahudumiwa wala kulipwa stahili zake na Bunge, wala Spika au kiongozi wa Bunge kwenda kumtembelea," alisema Mughwai.