BISMILLAH.
Eda ni muhula maalum ambao mwanamke, aliyekwisha olewa, anatakiwa kusalia bila ya kuolewa wala kuposwa kutokana na mojawapo wa sababu mbili kuu:
A. kutalikiwa\kuachwa au kuachika na
B. Kufiwa na mumewe (au mume kutoweka au kukimbia pasipo kujulikana aliko…).
Kwa maana hiyo, Eda ni muhula wa wajibu, uliofaradhishwa ndani ya Qur’ani Tukufu na Hadithi za Mtume ﷺ ambazo ziko nyingi. Mwenyezi Mungu anasema:
وَالْمُطَلَّقَاتُ يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ ثَلاَثَةَ قُرُوَءٍ وَلاَ يَحِلُّ لَهُنَّ أَن يَكْتُمْنَ مَا خَلَقَ اللّهُ فِي أَرْحَامِهِنَّ )
. وقوله تعالى (وَالَّذِينَ يُتَوَفَّوْنَ مِنكُمْ وَيَذَرُونَ أَزْوَاجاً يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْراً )
“Na wanawake walioachwa (watalikiwa): wangoje (wasiolewe) mpaka tohara tatu zishe. Wala haiwajuzii kuficha mimba aliyoumba Mwenyezi Mungu katika matumbo yao, ikiwa wanamuamini Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho”.Q;2.28.
“Na wale wanaofiwa na waume zao, miongoni mwenu na kuacha wake, wake hao wangoje (wakae eda) miezi mine na siku kumi.” Q.2:34.
Ama mja mzito aliyefiwa na mumewe, basi eda yake ni tokea tarehe ya kufa mumewe hadi ajifungue.
Vivyo hivyo, mtalikiwa mja mzito, eda yake ni hadi kujifungua.
Akijifungua tu basi eda yake imeisha.
(وَأُوْلَاتُ الْأَحْمَالِ أَجَلُهُنَّ أَن يَضَعْنَ حَمْلَهُنَّ ).
“Na wale waja wazito, basi muhula wao ni pale watapotua ujauzito wao.”
Ama mwanamke alieachwa kabla ya kujamiiana na mumewe, yeye hakai eda yoyote, na wala hana mahari –iwapo mahari hayo hayakutajwa kinaganaga-, isipokuwa kiliwazo (i.e. kiacha nyumba, yaani kitu cha kuanzia maisha ya ujane).
Lakini ikiwa kima cha mahari kilishatajwa na akaachwa kabla ya kujamiana na mumewe, basi mwanamke huyo, pamoja na kwamba hakai eda, anapaswa kulipwa nusu ya mahari ya kima kilichotajwa; ila kama yeye mwenyewe au walii wake (mzee wake, kwa mwanamwari) atasamehe malipo hayo Q.2;37. Na katika aya nyengine Q.33.49 Mwenyezi Mungu anasema:
(يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا فَمَتِّعُوهُنَّ وَسَرِّحُوهُنَّ سَرَاحاً جَمِيلاً )
“ Enyi mlioamini! Mtakapowaoa wanawame; wenye kuamini kisha mkawpa talaka kabla ya kuwagusa (kuingiliana kimwili), basi hamna eda juu yao mtakayoihisabu. Na wapeni cha kuwaliwaza na muwawache muachano mzuri” Q.33.49.
Ama mwanamke anayefiwa na mume basi eda yake ni miezi mine na siku kumi, kama nilivyotaja hapo juu na kunakili aya ya Qur áni. Na ni sawa ikiwa mume huyo alikwisha jamiiana na mkewe au la; mke atakaa eda ya miezi mine na siku kumi. Yaani, mfiwa na mume anakaa eda ya miezi mine na siku kumi. Iwapo ana mimba basi mpaka ajifungue.
Vile vile, mke huyo anamrithi mumewe huyo aliyefariki, awe aliingiliana naye kimwili au la. Kama mume hakuacha mtoto au watoto (kwa mke mwengine, kwa mfano) basi mwanamke atarithi robo ya mali yote ya mume na kama mume aliacha mtoto au watoto basi mke atarithi thumuni (one eighth) ya mali yote ya mume.
Hivyo ndivyo alivyoamua Mtume ﷺ kwa Sahaba mmoja aliyekuwa akiitwa: Ma’qal Ibn Yasar ambaye alifariki na kuacha mke kabla ya kuingiliana naye kimwili.
Hali kadhalika, Ibn Masúd – mmoja wa Maswahaba wakubwa- alikabiliwa na kesi kama hiyo ya mke kufiwa na mume ambaye bado hajaingiliana naye kimwili. Ibn Mas’ud akatoa fatwa ya mke kukaa Eda na pia kumrithi mumewe. Akapewa khabari kuwa Mtume ﷺ alitoa hukumu kama hiyo kwa Ma’qal Ibn Yasar! Ibn Mas’ud alifurahi sana kuona kuwa hukumu yake imewiana na hukumu ya Mtume ﷺ .
Pili, ni muhimu kujua kwamba mwanamke anakaa eda kwenye nyumba ya mumewe, awe mume yuhai au la, na katika muhula wote wa eda, mwanamke huyo anaendelea kulishwa kama kawaida kuktokana na mali ya mume, mpaka eda yake ishe. Mwenyezi Mungu anasema:
(لَا تُخْرِجُوهُنَّ مِنْ بُيُوتِهِنَّ وَلَا يَخْرُجْنَ إِلَّا أَنْ يَأْتِينَ بِفَاحِشَةٍ مُبَيِّنَةٍ ) الطلاق/1
“….Msiwatoe katika nyumba zao wala asitoke wenyewe, ila wakifanya jambo la ufasiqi ulio wazi. Na hii ni mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na anayekiuka mipaka ya Mwenayezi Mungu basi amejidhulumu nafsi yake. Hujui; (sababu ya kuamrishw hwaha): huenda Mwenyezi Mungu akazusha jambo jingine baad ya haya (yaani jambo la kupatana).” Q.65:2.
HEKIMA YA EDA.
Hakuna halali ambayo anaichukia Mwenyezi Mungu kama anavyochukia talaka.
Hii ni kwa sababu ndoa ni fungamanisho takatifu,, ni ahadi tu ya mdomo anayotoa mtu, mbele ya watu, kuwa yeye anafunga ndoa na fulani kwa JINA LA MWENYEZI MUNGU. Jina la Mwenyezi Mungu ndilo linalotumika kumtoa mtoto wa watu katika familia yake na kumuingiza katika familia nyengine kabisa. Hivyo, si jambo la kupendeza hata kidogo, bali ni jambo analolichukia Mwenyezi Mungu kumuona mja wake aliyetumia Jina la Mwenyezi Mungu kumuoa binti fulani na baadaye anaivunja ndoa hiyo na kumuacha! Anachukia Mwenyezi Mungu.
Lakini wakati huo huo, watu wawili wakeshaoana na ikafika hadi kuwa hawawezi kuvumiliana na kuishi pamoja basi hakuna haja ya kuwalazimisha kuishi maisha ya mateso na chuki na uhasama. Inakuwa, kwa wote wawili, kama wako jela katika nyumba yao ya ndoa! Hivyo basi, Kama walivyooana kwa salama na maelewano, wanatakiwa waachane kwa salama na maelewano; bila ya chuki, uhasama au dhuluma. Na ili kutoa nafasi ya kuja kutambua kuwa uamuzi haukuwa wa busara, au kwamba yumkini: mwanamke ana uja uzito, jambo ambalo ni jukumu la mume kumkimu na kumtunza, na kwa jamii kutambua kuwa mtoto atayezaliwa ni mtoto wa ndoa, basi ndipo pakawekwa muhula wa eda. Hivyo, tunaweza kusema kuwa hekima za eda ni nyingi. Miongoni mwake ni:-
a) Kutoa fursa ya kutafakari na kupima kwa walioachana, ili waweze kurudiana bila ya kufung ndoa tena.
b) Kujua kama fuko la uzazi lina mwana au la, na hivyo kulinda nasaba na koo na kuepuka kuchanganya vizazi visivyo husiana kidamu.
c) Kutunza na kuendeleza haki za urithi, kwa mujibu wa Quráni na Sunna za Mtume ﷺ
d) Kuisaidia jamii katika kujua na kutambua nasaba za koo ndani ya jamii, na hivyo kujua nani ana jukumu lipi, kabla ya jamii yenyewe kubeba jukumu kama hilo iwapo hakuna wa kulibeba.
e) Kutambua jukumu la utunzaji na kukimu familia analo nani? Yaani mume jukumu lake haliishi hadi pale itapojulikana wazi wazi kuwa hakuna kizazi chochote kati yake na aliyemuacha.
f) Kuwapa fursa wazazi na jamaa wa pande zote mbili kutafuta suluhu ya ndoa ya watoto au jamaa zao.
g) Kumpa fursa mwanamke aliyefiwa na mumewe kuwaliwaza wakwe zake na familia ya marehemu mume wake.
h) Kulipa uzito unaostahiki fungamanisho la ndoa katika jamii.
i) Kuonesha kuwa talaka si jambo la mchezo, mtu kuoa na kuacha tu, akidhani hana majukumu na dhamana hata baada ya kuacha.
Na mengi mengi mengine, ambayo haiwezekani kuyataja yote hapa.
والله أعلم
وبالله التوفيق
السيد عبد القادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم
Imejbiwa na Sayyid Abdulqadir Shareef
NI RUHUSA KUNUKUU, kama ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza chchote, na kuweka kwenye FB yako au kwenye WhatsApp na kwenye Makundi ya Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, kwa lengo la kusambaza na kuelimisha Dini. Changia kusambaza Dini, ujipatie thawabu.