ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Simba Mcameroon, Joseph Omog, amegoma kuondoka jijini Dar es Salaam akisubiria malipo yake kutoka kwa mabosi wake wa zamani.
Awali, kulikuwepo na taarifa za kocha huyo kuondoka jana lakini imeshindikana mara baada ya viongozi wa timu hiyo kumsitishia mkataba wake wa kuendelea kuifundisha Simba.
Simba ilimsitishia mkataba huo kocha huyo mara baada ya matokeo mabaya waliyoyapata dhidi ya Green Warriors inayoshiriki Ligi Daraja la Pili katika hatua ya pili ya Kombe la FA.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, kocha huyo yupo nyumbani kwake Kunduchi Beach jijini Dar es Salaam anapoishi akisubiria
malipo hayo ya fedha kutoka kwa mfanyabiashara, Mohamed Dewji ambaye amekabidhiwa kuiongoza klabu hiyo.
Mtoa taarifa huyo alisema, kocha huyo ameahidiwa kupewa malipo yake ya fedha hizo kuanzia leo Jumatatu hadi Jumatano atakuwa amepatiwa na tayari kuanza safari ya kurudi kwao.
Aliongeza kuwa, tayari wamefikia muafaka mzuri wa kumlipa kocha huyo kwa kipindi cha takribani miezi sita alichokibakiza tangu asaini mkataba wa miaka miwili ya kuifundisha Simba.
“Kuna picha zinaenea zikimuonyesha Omog ameondoka, niseme kuwa siyo ukweli bado yupo nchini akisubiria malipo yake ya fedha ya mkataba wake wa miezi sita alioubakisha.
“Hivyo, basi amepanga kuondoka nchini kati ya Jumatatu au Jumatano ya wiki ijayo baada ya kupatiwa
fedha hizo, kama unavyojua kesho Jumatatu ni sikukuu ya Krismasi, hivyo benki zote zitakuwa zimefungwa.
“Hivyo viongozi hao wamemtaarifu kuwa malipo yake yatafanywa kuanzia wiki ijayo mara baada ya sikukuu hiyo kumalizika ndiyo ataondoka akiwa amekamilisha kila kitu chake,” alisema mtoa taarifa.
Alipotafutwa Kaimu Makamu wa rais wa timu hiyo, Iddy Kajuna kuzungumzia hilo simu yake ya mkononi iliita bila ya mafanikio ya kupokelewa.
Alipotafutwa Omog jana mchana alisema hataki kuzungumza chochote kuhusiana na Simba lakini akasisitiza yupo jijini Dar na ataondoka muda wowote baada ya kumalizana na Simba kuhusiana na malipo yake.
“Kuhusu Simba sitaki kuzungumza chochote rafiki yangu, nitaondoka baada ya kumalizana na uongozi,” alisema kwa ufupi Omog.