GARI la Jeshi la Polisi linalobeba maji ya kuwasha maarufu kama ‘washawasha’ lililokuwa kwenye msafara wa kusindikiza mahabusu, lilipinduka barabarani na kusababisha msongamano wa magari katikati ya Jiji la Dar es Salaam jana.
PICHA HII HAIHUSIANI NA HABARI HII.
Washawasha hilo lenye namba PT 0887 aina ya Mercedes Benz, ambalo ndani yake kulikuwa na dereva na askari mmoja, lilipata ajali Barabara ya Bibi Titi, baada ya tairi moja la mbele kupasuka.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alithibitisha kuwapo kwa ajali hiyo iliyotokea saa 4:00 asubuhi na kutaja chanzo chake kuwa ni kupasuka kwa tairi.
“Baada ya ajali ilifanyika juhudi za kuliinua na kuliondoa eneo la barabara ili lisiendelee kusababisha foleni zaidi katikati ya mji,” alisema.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Hamduni alisema gari hilo lilikuwa likitokea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuelekea Kambi ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Ukonga.
“Gari hili la washawasha lilikuwa kwenye mwelekeo mmoja na magari mengine ambayo yalikuwa yamebeba mahabusu wakitoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuelekea Ukonga,” alisema.
Alisema baada ya kufika eneo hilo ndipo lilipopinduka na kusababisha barabara hiyo isipitike pamoja na kuwajeruhi askari waliokuwa ndani.
Alisema waliojeruhiwa ni dereva na askari mmoja aliyekuwa ndani ya gari hilo ambalo nalo limeharibika.
“Ajali ilitokea saa 4:00 asubuhi na hadi saa 5:15 lilikuwa limeshaondolewa eneo la tukio, ilichukua muda kidogo kuliondoa kama unavyojua uzito wa gari hili,” alisema.