Imeelezwa kuwa ujenzi wa mitambo ya kuzalisha Umeme wa kiasi cha megawati 240 kwa kutumia Gesi Asilia katika mradi wa Kinyerezi II umefikia asilimia 84.
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam na Meneja Miradi ya Umeme ya Kinyerezi, Mhandisi Stephen Manda wakati akitoa taarifa ya miradi ya Kinyerezi I (MW 150), Kinyerezi I-Extension (MW 185) na Kinyerezi II (MW 240) kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.
Naibu Waziri Mgalu alifanya ziara katika mitambo hiyo lengo likiwa ni kupata taarifa na kukagua kazi iliyofanywa na Wataalam wa TANESCO ya kusafisha na kuunga Bomba kubwa la Gesi katika mitambo ya Kinyerezi I iliyofanyika Novemba 18 na 19 mwaka huu na hivyo kusababisha upungufu wa Umeme katika gridi ya Taifa.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli hiyo, Mhandisi Manda alieleza kuwa TANESCO walikamilisha zoezi hilo kwa ufanisi na ilipofika mchana wa Novemba 20, 2017 mitambo hiyo iliingiza megawati 115 katika Gridi ya Taifa na hivyo kuboresha hali ya upatikanaji wa Umeme.
Kuhusu mradi wa Kinyerezi II unaotekelezwa na Mkandarasi SUMITOMO kutoka nchini Japan, Mhandisi Manda alisema kuwa matarajio ni kuanza kuzalisha Umeme mwanzoni mwa mwezi Disemba mwaka huu ambapo megawati 30 zitaanza kuingizwa katika Gridi ya Taifa.
Aidha, alisema kuwa, matarajio ni mitambo hiyo kuongeza megawati 30 kwenye gridi ya Taifa kila mwezi mpaka zitakapokamilika megawati 240 mwezi Julai, 2018.
Alieleza kuwa, Mkandarasi wa mradi huo anatarajia kukabidhi mradi husika kwa Serikali Septemba 30, mwaka 2018 na kuongeza kuwa Wataalam wazawa watakaoendesha kituo hicho tayari wamepata mafunzo kutoka nje na ndani ya nchi.
Kuhusu utekelezaji wa mradi wa Kinyerezi I-Extension (MW 185), alisema kuwa utekelezaji wake umefikia asilimia 48 na kwamba ujenzi wa misingi yote ya mitambo na viambata vyake imekamilika.
Aliongeza kuwa, mitambo yote ya Umeme itakayotumika kwenye mradi huo imeshatengenezwa na ipo tayari kuletwa nchini baada ya kukaguliwa na wataalam na kwamba Wataalam wa TANESCO wapo nchini Norway kwa ajili ya kukagua mifumo ya uendeshaji wa mitambo hiyo kabla kusafirishwa kuja nchini.
kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati aliwapongeza wataalam wa TANESCO kwa kusimamia kwa umakini miradi hiyo na kuwataka kuendelea kufanya kazi usiku na mchana ili kuweza kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.