SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 9 Novemba 2017

T media news

Tamko la Waziri wa Elimu Bungeni Kuhusu Mikopo

Serikali imewaagiza wakuu wote wa vyuo vya elimu ya juu kuacha urasimu katika utoaji wa fedha kwa wanufaika wa mikopo ambao wana makubaliano na Serikali.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema leo bungeni ikiwa ni utekelezaji  wa agizo la Spika Job Ndugai  lililotaka serikali kutoa kauli kuhusu wanafunzi wa mwaka wa kwanza kutakiwa kutoa fedha ili wasajiliwe kabla ya kupata  mikopo.

Agizo la Spika lilitokana na Mwongozo uliombwa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Martha Mlata ambaye alieleza bunge kuwa wanafunzi wamekuwa wakihangaika vyuoni baada ya kutakiwa walipe fedha za usajili kabla ya kupewa mkopo.

"Serikali imeshawaagiza wakuu wa vyuo vya elimu ya juu kuacha urasimu katika utoaji wa fedha kwa wanufaika kwa mikopo ambao wana makubaliano na Serikali," amesema.

Amesema inasikitisha sana kuona baadhi ya vyuo vinadiriki hata kuwakataa wanafunzi waliowadahili wao wenyewe au vinawalazimisha wachukue programu tofauti na walizokuwa wamechaguliwa awali na vyuo husika.

" Jambo hili halikubaliki hata kidogo na linaleta shaka kuhusu uadilifu wa vyuo husika. Naiagiza TCU (Tume ya Vyuo Vikuu) na Kurugenzi ya Elimu ya Juu ya Wizara, kufuatilia kwa karibu mambo yote yanayopendelea vyuoni wakati wanafunzi wanaripoti na kubainisha wote wanaokiuka taratibu na kuwanyima wanafunzi haki yao ya kusoma programu wanazoitaka," amesema.

Amesema Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa vyuo vyote vitakavyoleta usumbufu usio wa lazima kwa wanafunzi na kuwafanya wapoteze muda ambao wanapaswa kuutumia kwa masomo.