SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 9 Novemba 2017

T media news

Ndoa ya Uwoya, Dogo Janja Yamuibua Mr Nice

Unapozungumzia wakongwe wa muziki wa Bongo Fleva waliowahi kutusua, huwezi kumuacha Lucas Mkenda ‘Mr Nice’.
Kwa mfuatiliaji wa burudani Bongo atakuwa anazikumbuka kufuru za Mr Nice mjini alizokuwa akizifanya baada ya kupata mafanikio makubwa ya kimuziki. Alifuja mkwanja kiasi cha kuzurura mitaa ya jijini Dar akiwa na magari ya kifahari huku akitembea na warembo kadhaa kwenye kila viwanja vya starehe.

Fedha kwake ilikuwa si tatizo. Ndiye muasisi wa staili ya Tanzania, Kenya and Uganda almaarufu Takeu.

Alisumbua vilivyo na nyimbo kama Kikulacho, Rafiki na nyingine nyingi ambazo ziliamsha hisia na kupendwa na wengi.

Baadaye alipotea kwenye gemu, zile vurugu zote zikawa zimekwisha! Nini tatizo? Alikosea wapi?

Vipi kuhusu anachokifanya kwa sasa, makazi yake na mambo mengine mengi? Mara paap! Mr Nice huyu hapa anafunguka yote katika mahojiano maalum na gazeti bora la mastaa Bongo;

Amani: Niaje Nice, naona umerudi tena, vipi, una ujio mpya?

 

Mr Nice: Yaaa! Ni kweli nimeachia ngoma mpya inayokwenda kwa jina la Yaya. Ngoma hii nimeifanya kwa prodyuza Eck.

Amani: Je, umekuwa unakumbana na changamoto gani kiasi kwamba umekuwa unatoa ngoma na kupotea?

Mr Nice: Si kweli. Kwanza mimi sijapotea, labda kwenye ‘media’ tu za hapa nyumbani (Bongo), lakini huwezi kuamini, ninafanya shoo za kufa mtu nje ya Bongo.

 

Amani: Kwa nini umekuwa ukifanya shoo zaidi nje ya Bongo kuliko hapa nyumbani? Siyo kwamba unakimbia changamoto za soko la muziki kwa sasa ambazo zimewakumba wakongwe wengi?

Mr Nice: Kwanza niweke wazi kwamba, kwa sasa makazi yangu ni nje ya nchi na hapa Tanzania panabaki kuwa nyumbani tu. Mimi ninaishi Kenya. Kwa hiyo shughuli zangu za muziki na biashara zangu zote nimeweka ‘base’ huko. Lakini kuhusu kufanya shoo nje ya nchi, jibu ni rahisi tu, kwamba, kila mfanyabiashara hutazama chaka linaloweza kumuingizia fedha na ndiko hupeleka bidhaa zake.

Si kwamba nimekimbia changamoto za muziki, maana siku hizi hakuna changamoto.

Amani: Kwa nini unasema hakuna changamoto?

Mr Nice: Kwa sababu muziki tulishaufanya ueleweke. Changamoto zilikuwa kitambo wakati sisi tunawafanya watu waelewe kwamba muziki si uhuni, bali ni fursa ya kibiashara.

 

Amani: Hivi karibuni uliingia kwenye ‘headlines’ baada ya kuonekana kwenye video ya mwanamuziki mmoja nchini ukiwa kama ‘video model’, kwako mapokeo ya hiki ulichokifanya kwa Watanzania unayachukuliaje?

Mr Nice: Nachukulia kwamba ni ushamba tu kwa watu walioponda kile nilichofanya. Kwa maana tumeona kwa nchi zilizoendelea wanamuziki wakubwa wanafanya hivyo. Imeshafanyika kwenye video kama za akina Nick Minaj na wengine wengi. Kwa hiyo Watanzania waamke tu.

 

Amani: Suala la malipo kwako kwa sasa likoje maana kipindi cha nyuma ulikuwa ni mwanamuziki unayelipwa mkwanja mrefu zaidi kuliko mwanamuziki yoyote wa Bongo Fleva?

Mr Nice: Lipo kawaida, bei ni maelewano na huwezi kuzuia upepo unap

obadilika. Hata Mike Tyson alikuwa ni bondia aliyelipwa kuliko mwanandondi yoyote yule, lakini siku hizi tunaona akina Floyd Mayweather ndiyo wamechukua nafasi. Kwa hiyo muda unapobadilika, huwezi kuuzuia. Nina furaha kwa sasa kwa mwanamuziki yeyote anayelipwa kuliko mimi.

 

Amani: Una nini cha kuzungumzia kuhusu wadogo zako wa sasa namna wanavyofanya muziki, tumeona Aslay anatoa wimbo mpya kila mwezi, je, una lolote la kukomenti?

 

Mr Nice: Kubwa ni kumpa tu changamoto mdogo wangu, Aslay, kwamba, kwa namna anavyofanya muziki wake ni yeye mwenyewe anaua nyimbo zake.

Ndani ya mwezi mmoja huwapi mashabiki nafasi ya kusikiliza wimbo vizuri, unapotoa wimbo mpya kila mwezi unawachanganya akili na kufanya waurukie huo mpya na kuutupa uliotangulia. Kwa hiyo hilo aliangalie, lakini pia aangalie kuhusu anguko lake.

 

Wanamuziki hatutambi muda wote, sasa kwa staili yake inawezekana kabisa akaja kukosa jipya atakapoanguka kimuziki.

Amani: Kwa sasa kiki ndiyo kila kitu mjini. Ili uweze kuvuma na kupata ‘coverage’ ni lazima utengeneze kitu cha kuzungumziwa, kwako hili limekaaje?

 

Mr Nice: Halijakaa vizuri na ningependa jamii kulikemea kwa nguvu zote. Kwa mfano, hiyo kiki ya Irene Uwoya na Dogo Janja kwamba wameoana na si kweli, si suala zuri.

 

Unatumia nguvu kubwa kuwaaminisha watu kwamba mmeoana halafu kirahisi tu inagundulika kwamba si kweli. Ukweli ni kwamba huu si mfano wa kuigwa.

 

Amani: Kwa kumalizia unawaambia nini mashabiki wako pengine kuhusu familia yako, umeoa? Vipi kuhusu watoto pia?

 

Mr Nice: Nakushukuru pia, mimi sijaoa na sina mpango wa kuoa kwa sasa. Ninalea familia yangu tu maana nina watoto watatu, mkubwa anaitwa Colin (miaka 13), mwingine anaitwa Hairuni (12) na wa mwisho ni Gift na ana miaka minne kwa sasa. Hawa ndiyo macho yangu!

Chanzo: Global Publishers