SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 10 Novemba 2017

T media news

Spika Ndugai Awapa Rungu Wabunge wa CCM Kuikosoa Serikali

Spika wa Bunge, Job Ndugai amewapa rungu wabunge wa CCM akiwataka wafunguke wakati wa mijadala na si kusimama na kupongeza tu.

Spika alitoa kauli hiyo jana wakati wa kujadili mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/19 na mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti kwa mwaka 2018/19.

Kauli ya Spika ilitokana na mchango wa Peter Serukamba (Kigoma Kaskazini –CCM) ambao kwa kiasi kikubwa ulionyesha namna hali ya uchumi si nzuri na kutoa takwimu zinazoonyesha kushuka kwa uchumi nchini.

“Katiba iliweka utaratibu kwamba mipango ya nchi itapita hapa kwanza ninyi muijadili. Halikuwekwa hivyo kwa bahati mbaya. Liliwekwa hivyo ili nyinyi mseme kwa niaba ya wananchi,” alisema Spika.

Alisema, “Katika mambo ya msingi kama haya fungukeni. Msijifunge funge hapo ooh mimi CCM. CCM haitaki mipango mibovu. Ni wakati wenu wa kusema tumsaidie waziri na tuisaidie Serikali ili tusonge mbele.”

Huku akipigiwa makofi na wabunge wa upinzani na wale wa CCM, Spika alisema “Na unapoomba nafasi ya kusema hapa uwe umejiandaa. Si ile tu naunga mkono nafanya hivi unakaa chini”.

Wabunge wawili wa CCM, Hussein Bashe wa Nzega na Serukamba jana walivaa ujasiri na kueleza waziwazi kuwa uchumi uko hatarini kuporomoka, huku Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe yeye alienda mbali na kudai Serikali inatoa taarifa za uongo, akisisitiza uchumi hautajengwa kwa mtutu wa bunduki, ubabe na vitisho.

Katika mchango wake, Serukamba ambaye alionekana kama kuwafungulia njia wabunge wa CCM, alisema mipango yote mitatu ni kama imeigizwa akitumia neno la ‘copy and Paste’.

“Ukipitia yote wamebadilisha lugha lakini kinachosemwa ni kilekile. Deni la Taifa linapanda kwa Sh4 trilioni kwa mwaka. Maana yake tumeamua kama Serikali kila kitu kinafanywa na Serikali,” alisema.

“Hatuwezi kuendelea. Halipo Taifa duniani ambalo kila kitu wanajenga kwa fedha za Serikali. Tumekwenda Moscow uwanja wa ndege wa kimataifa umejengwa na mtu binafsi.”

Serukamba alisema Serikali inasema inatekeleza miradi kwa ubia na sekta binafsi (PPP), lakini katika kitabu cha waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango hakuna mradi ulioonyeshwa.

“Serikali hii haiamini katika sekta binafsi. Nataka Bunge hili tukubaliane Waziri wa Fedha atuambie, Serikali hii haikubaliani na Sekta binafsi. Kama tumerudi kwenye ujamaa tuambiane,” alisema.

“Namuonea huruma sana Rais. Anahangaika lakini wenzake hawamwambii ukweli. Humu ndani waziri anaongelea kukusanya kodi peke yake. Tunakusanya kodi kwa nani?”

“Leo mabenki yanakufa. Mabenki yote yanaonyesha kushuka kwa faida. Hata mabenki makubwa. Hata uchumi unaofanya vizuri tunaangalia ufanisi wa sekta ya mabenki na ufanisi wa soko la mitaji”

“Nchi ni yetu sote. Haiwezekani viwanja vya ndege tujenge kwa pesa zetu, reli tujenge kwa pesa zetu, umeme pesa zetu, barabara kwa pesa zetu sisi ni nani. Dunia yote imeenda kwenye sekta binafsi”

“Leo ukienda kwenye mabeki kila kitu kimeshuka. Personal lending (mikopo kwa wafanyakazi) mwaka 2015 ilikuwa asilimia 25.5 leo ni asilimia 8. Mikopo ya biashara mwaka 2015 ilifika asilimia 24.6 leo ni asilimia tisa 9.”

“Hakuna anayesema na tukisema utaanza kupewa majina. Mambo hayako sahihi kwa sababu moja tu, mpango wetu wa mwaka huu ndiyo wa mwaka jana na ndio wa mwaka juzi,” alisisitiza Serukamba.

Akizungumzia hilo, Bashe alisema vigezo vya kupima uchumi wowote duniani una kioo na kioo cha uchumi wowote unaokua au kusinyaa au unaoshuka ni taasisi za fedha, biashara na soko la mitaji.

Alisema mikopo kwa watu binafsi imeshuka hadi asilimia 8.9 mwaka huu kutoka asilimia 25 za mwaka 2015 huku mikopo ya kibiashara nayo ikishuka hadi asilimia tisa kutoka 24 za mwaka 2015.

“Na maneno haya siyatoi pengine ni report za BoT (Benki Kuu ya Tanzania) inayoishia Juni mwaka huu. Kilimo leo ni negative 9 (hasi) kutoka asilimia sita. Manufacturing kutoka asilimia 30 hadi tatu,” alisema.

“Uchumi wetu unasemwa unakua kwa asilimia 6.8 lakini taarifa ya mwisho niliyonayo inasema asilimia 5.7,” alisema Bashe huku akisisitiza kuwa Serikali haijajipanga katika kutekeleza mpango huo.

“Waziri katika kitabu chake hiki anasema watafanya uhimilishaji wa mifugo 459,000 na tunapanga kuzalisha hay (majani ya ng’ombe) 445,000 kitakwimu hay moja ina uzito wa kilo 25”.

“Chakula hiki ukikigawa kwa siku 365 kinalisha ng’ombe 1,600 tu. Huku unapanga kuzalisha ng’ombe 400,000 lakini unaandaa chakula cha kulisha ng’ombe 1,600?”alihoji Bashe.

Alisema mapinduzi ya viwanda hayawezekani bila kuwekeza katika sekta ya kilimo na kwamba, Serikali inajaribu kudhibiti mfumuko wa bei kwa kuwatia umasikini wakulima.

“Yaani tunadhibiti mfumuko wa bei kwa kumtia umasikini mkulima. Aina gani za economy (uchumi) hizi? Waziri amejikita kwenye kodi tu badala ya kujikita kwenye uzalishaji,” alisema.

Bashe alisema katika kitabu chake, waziri Mpango ameeleza namna miradi itakavyofaliwa kuwa ni pamoja na kuboresha mashine za kielektroniki (EFD) na kuanzisha maabara ya TRA.

“Haumsikii akisema tutawekeza bilioni moja kwenye kilimo cha mahindi ili tuweze kupata. Huwezi kukamua maziwa ng’ombe usiyemlisha,” alisema Bashe.

Alisema, “VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) na PAYE (lipa kadri unavyopata) zimeshuka yeye anasema ni kwa sababu kampuni zimepunguza wafanyakazi.”

Bashe alisema katika kamati ya bajeti walimshauri Waziri Mpango kutoongeza kodi katika viwanda vya bia na vinywaji baridi kwa vile ingepunguza uwezo wa uzalishaji lakini hakuwasikiliza.

Akichangia katika hilo, Mbowe aliwapongeza Serukamba na Bashe kwa kuwa wa kweli na kueleza kuwa wabunge hawataisaidia nchi kama watakuwa wanafiki na kusema wataisaidia kwa kuikosoa pale inapofaa kuikosoa.

“Tutaisaidia nchi hii kwa kuwa wa kweli na kukosoa katika mambo ambayo ni lazima. Tupongeze pale panapostahili. Tusipoikemea Serikali na kuiambia ukweli,” alisema.

Mbowe alisema, “Kwamba wale wanaosema ukweli wanastahili kufa, wale wanaoikosoa Serikali wanastahili kuumizwa hatutafika. Chama chochote cha siasa kikifikia mahali pa kutotaka ushauri lazima kife.”

“Maumivu yanapotokea kwa wananchi ninyi CCM ndio mnawajibika kuanzia Rais, mawaziri na wabunge wa CCM. Ninachoona kinafanyika kwa juhudi sana ni kuirudisha nchi kwenye Ujamaa,” alisema Mbowe.

Alisema, “Mahusiano kati ya Serikali na Sekta binafsi sio mazuri. Hatutajenga uchumi wa nchi hii kwa mtutu wa bunduki. Hatujengi uchumi wa nchi hii kwa ubabe na vitisho. Ni lazima Serikali itambue kuwa sekta binafsi ndio injini ya uchumi na serikali ni bodi. Hakuna taifa lolote limeendelea duniani kwa kuipuuza sekta binafsi.”

Alisema, “Hakuna Taifa lolote duniani liliendelea kwa kufikiria sekta binafsi ni wezi. Kufanya biashara nchini hii chini ya awamu ya tano ni kiama. Wafanyabiashara wote wa ndani na nje wanalia.”

“Leo Rais anahimiza viwanda ili mwaka 2025 iwe nchi yenye uchumi wa kati. Huwezi kujenga viwanda kwa kutegemea soko lako la ndani ni lazima utegemee masoko ya nchi jirani. Lazima tufungue mipaka Lakini ukitizama mahusiano yetu na nchi za Afrika Mashariki tunafunga mipaka. Tunachoma vifaranga, tunapiga mnada ng’ombe za watu,” alisema.

“Kuna suala la utawala bora. Ukizungumza na kuchambua uchumi leo unashitakiwa . Sisi wapinzani tufanye nini? Serikali inatoa takwimu za uongo. BoT inatoa takwimu zinazotofautiana na za wizara”

“Kama tusipojipa ujasiri wa kuikosoa Serikali pale inapobidi, msiba utatuumbua. Hali yetu ya uchumi ni ngumu. Uchumi si Fly Over au Bambadier sita. Uchumi ni kipato kwa wananchi wa kawaida,” alisema Mbowe.

“Watanzania wanazidi kuwa masikini na kundi dogo ndio linaona kukua kwa uchumi wa taifa. Kukua kwa uchumi tunakoambiwa hakuoani na maisha ya watanzania. Watanzania wanazidi kuwa masikini”

Hata hivyo, katika mchango wake, Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa alimtaka waziri Mpango kuacha tabia yake ya kiburi (arrogance) kwa vile tabia hiyo haisaidii Serikali.

“Sina uhakika hata kama simu za wabunge unapokea. Jitahidi kusikiliza kamati za bajeti. Ukiendelea hivyo iko siku utakwama na utakaporudi kwetu na sisi hatutakusikiliza,” alisema.

“Wewe si msikivu kwa wabunge. Jaribu kubadilika sisi wote tuko kwenye boti moja na hakuna ambaye anataka kutoboa boti. Sisi ni wabunge wenzako. Sikiliza ushauri,”.

Mjadala huo utaendelea hadi Jumatatu ijayo na baadaye Bunge litaingia katika kupokea miswada mbalimbali ukiwamo muswada wa kuanzisha Wakala wa Meli Tanzania wa mwaka 2017.