SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 8 Novemba 2017

T media news

Serikali yatoa Hekta 271,882.86 kwa Ajili ya Shughuli za Vijana

Na Lilian Lundo, Dodoma

 Serikali kupitia Halmashauri za Wilaya katika mwaka 2016 imetoa jumla ya  Hekta 271,882.86 za ardhi kwa vijana nchi nzima ili kufanya shughuli za uzalishaji mali na kujipatia ajira.

Hayo yameelezwa jana, Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana na Watu Wenye Ulemavu Anthony Mavunde alipokuwa akijibu swali la Mbunge Viti Maalum Mhe. Aida Khenan juu ya mpango wa Serikali kwa vijana wanaomaliza shule za msingi, Sekondarii na Vyuo kwa kuwazesha kujiajiri.

“Serikali imeendelea kuimarisha utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao unalenga kuwasaidia vijana wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu kuweza kujiajiri kwa kuwapa mikopo ya masharti nafuu na mafunzo ya ujasiriamali,” alisema Mavunde.

Aliendelea kwa kusema, katika kipindi cha mwaka 2013/2014 hadi 2016/17, Serikali kupitia mfuko wa Maendeleo ya vijana imetoa mikopo ya masharti nafuu ya Shilingi Bilioni 5.8 kwa vikundi vya vijana 6,076 vyenye wanachama 30,380 katika Halmashauri za Wilaya 157 kupitia SACCOS za Vijana.

Aidha Mavunde alisema, kupitia programu ya kukuza ujuzi wa nchi Serikali imeanzisha utaratibu maalum wa kutambua ujuzi uliopatikana kupitia mfumo usio rasmi na kuurasimisha kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wale walio tayari kuhitaji na kuwapa vyeti vinavyotambulika.

“Utaratibu huu unawapafursa vijana wetu ya kuendelea na mfumo rasmi wa mafunzo na pia kutambulika na waajiri au watoa kazi,”� alifafanua Mavunde.

Vilevile alisema, Serikali imerahisisha utaratibu wa uundaji wa Makampuni kupitia BRELA hivyo vijana wengi wanaomaliza vyuo kuweza kuanzisha Makampuni na biashara zinazowezesha kuajiri vijana wengi.

Hata hivyo, Mavunde amewataka vijana wanaomaliza shule za msingi na sekondari kujiunga katika vikundi vya kuzalisha mali na kusajiliwa rasmi kupitia sheria ya usajili wa NGOs.

Aidha mpaka sasa jumla ya vikundi vya vijana vya uzalishaji mali 10, 200 vimesajiliwa.