Mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania anayekipiga katika klabu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji, Mbwana Ally Samatta atalazimika kukaa nje ya uwanja kwa kipindi cha miezi sita baada ya kupata majeraha wakati akiitumikia klabu yake.
Samatta aliumia Jumamosi wakati KRC Genk alipokuwa ikiikabili Lokeren katika mchezo wa ligi kuu ambao ulimalizika kwa timu zote kutoka suluhu.
Katika mchezo huo, Samatta alidumu uwanjani kwa muda wa dakika 40 kabla yakutolewa nje kwa kujeruhiwa mguu.
Samatta ambaye pia ni Nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars hatakuwa katika kikosi cha Stars kitakachocheza dhidi ya Benin kwenye mchezo wa kirafiki utakaopigwa Novemba 12 mwaka huu nchini Benin.
Licha ya Samatta kuwa majeruhi, wachezaji wengine wa Stars pamoja na kocha Salum Mayanga wameahidi kupata ushindi kwenye mchezo huo kitu ambacho wanaamini kitakuwa faraja kwa nahodha wao.