SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 14 Novemba 2017

T media news

Lawrence Masha ajivua uanachama Chadema

Aliyekuwa mwanachama CCM, ambaye baadaye alihamia Chadema, Lawrance Masha amejivua uanachama katika chama hicho akidai  upinzani wa sasa umeridhika na hali ya kuendelea  kuwa wakosoaji ili kukisaidia chama tawala kujirekebisha.

Pia amesema, “Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa upinzani wa sasa nchini hauna nia wala sababu ya kutafuta fursa ya kuunda Serikali kupitia falsafa, sera na uongozi mbadala.”

Masha ameeleza hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa leo Jumanne Novemba 14.

Masha ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, katika Serikali ya awamu nne, amesema upinzani hauwezi kutegemea kushika dola kwa kutegemea madhaifu ya CCM badala uwezo wake kama mbadala.

Amesema  kazi kubwa ya chama chochote cha siasa ni kujiandaa na hatimaye kushinda uchaguzi ili uweze kuunda na kuendesha Serikali na dola kama njia ya maono yaliyo kwenye ilani ya uchaguzi kwa lengo la kuleta maendeleo na ustawi katika nchi.

“Nilijivua uanachama CCM mwaka 2015 na kujiunga Chadema nikiamini nitashiriki kukifanya chama hiki kikomae na kufikia hatua ya kuwa mbadala kifalsafa, kisera na uongozi. Hata hivyo uzoefu wangu wa miaka miwili ndani ya Chadema umenionyesha chama hiki kina safari ndefu kisiasa na kuwa chama mbadala cha kuunda Serikali.

“Mpaka sasa chama hiki kimendelee kujikita katika kukosoa na kuonyesha madhaifu ya Serikali hasa Rais John Magufuli binafsi. Natambua kwamba kukosoa ni kazi muhimu ya chama cha upinzani, kazi hii haikifanyi chama kuwa mbadala cha kuunda Serikali,”amesema Masha katika taarifa hiyo.

Masha ambaye aliwani kuwa Mbunge wa Nyamagama mwaka 2005-10, amesema siyo sahihi kwa vyama vya upinzani kuwekeza katika kumpinga Rais Magufuli ambaye ni mkuu wa nchi pekee anayetekeleza kwa vitendo mambo ambayo upinzani ilikuwa ikiyapigia kelele kwa miaka mingi, na kuwashinda viongozi wa CCM  waliomtangulia.

“Nimejivua uanachama kuanzia leo, nina imani uamuzi huu utanipa fursa ya kutafakari kwa kina safari yangu ya kisiasa ndani ya nchi hii. Nawashukuru viongozi wa Chadema kwa miaka miwili ya kufanya kazi pamoja nao nawatakiwa kila la kheri,” amesema Masha ambaye alikuwa ni miongoni mwa watu walioshirikia kampeni za uchaguzi za mwaka 2015 kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).