ZAIDI ya wanafunzi 70 wanaosoma katika Shule ya Sekondari ya Nandembo wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma, wamekosa mahali pa kulala na kuhamishiwa eneo la kanisa, baada ya moto kuteketeza bweni lao.
Wanafunzi hao walinusurika kifo kutokana na kuwa darasani moto huo ulipoanza kuwaka Jumatatu.
Moto huo uliunguza na kuteketeza madaftari, nguo, mashuka na mali nyingine za wanafunzi.
Mashuhuda walisema bweni hilo walilokuwa wakilala wanafunzi wa kiume wa kidato cha kwanza na kidato cha nne lililipuka moto kati ya saa 1:30 na saa 2: 00 usiku.
Mkuu wa shule hiyo, Mary Ndunguru, alisema baada ya kuzuka kwa moto huo, walimu walishirikiana na wanafunzi kuuzima moto huo bila mafanikio.
Alisema wakati wa tukio hilo, wanafunzi walikuwa wakiendelea na masomo ya jioni katika madarasa yaliyopo zaidi ya mita 200, hivyo kuchelewa kubaini kilichokuwa kinaendelea.
Ndunguru alieleza baada ya kuudhibiti moto na kubaini kutokuwapo uwezekano wa wanafunzi kuendelea kulala katika bweni hilo, aliwasiliana na viongozi wa Kanisa Katoliki kijijini hapo na kuomba wanafunzi waende kulala eneo la kanisa kwa muda wakati uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ukiendelea na juhudi za kutafuta ufumbuzi wa kuwajengea bweni lingine.
Kaimu Ofisa Elimu wa Shule za Sekondari wilayani Tunduru, Habiba Mfaume, alisema takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya wanafunzi 72 walikuwa wanalala katika bweni hilo na hakuna aliyepata madhara.
Alisema amemuagiza mkuu wa shule hiyo kuwaita wazazi wote katika kikao kilichopangwa kufanyika kesho, ili kuomba msaada wa awali kwao na kila mzazi ajitahidi kufika na nguo zitakazosaidia kuwasitiri watoto wao katika kipindi hicho cha mpito.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Chiza Marando, alisema ili kuwasaidia wanafuzni wanaojiandaa kufanya mitihani ya kuhitimu masomo ya kidato cha nne inayotarajiwa kuanza Oktoba 30 mwaka huu, ameshawatuma wataalamu kupitia masomo yote waliyosoma, ili kuwasaidia kuwatolea nakala wanafunzi wote kuwasaidia waendelee kujisomea.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Tunduru ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Kaimu Ofisa Tawala wa wilaya hiyo, Agustino Maneno, alisema amemuagiza Kamanda wa Polisi wa wilaya hiyo kupeleka wataalamu wake kupeleleza chanzo cha moto huo.