Mchungaji Samwel wa Kanisa la ‘Free Pentekoste Church of Tanzania’ lililopo mkoani Morogoro ameuawa na muumini wake aliyedaiwa kuwa na mapepo wakati akimuombea.
Ndugu wa mchungaji huyo alieleza kuwa muumini huyo anayejulikana kwa jina la Nuhu Ayoub alikuwa akisumbuliwa na mapepo na akaletwa kanisani hapo ili kuombewa na mchungaji huyo na wakati maombezi yakiendelea ndipo alipotenda tukio hilo.
“Siku ya Jumapili alikuja kufanyiwa maombezi pale lakini kwa kuwa hali yake ilikuwa bado haijatengamaaa, ndugu zake wakaomba akae pale kanisani pale kwa mchungaji ili aendelee kuwa anafanyiwa huduma. Siku ya Jumanne alikuwa kwenye ibada vizuri na alikuwa na akili zake sawa sawa yuko vizuri tu. Ndiyo sasa hapo tukio lilipotokea halafu akaanza kumshambulia. Na wakati akimshambulia mzee hapakuwa na watu…,” alisema ndugu wa mchungaji huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na polisi kwa ajili ya uchunguzi na atachukuliwa hatua baada ya uchunguzi kukamilika.
“Samwel Mchungaji wa Kanisa la Free Pentecostal church of Tanzania akiwa kanisani alishambuliwa na mtuhumiwa mmoja anayejulikana kwa jina la Nuhu na kusababisha kifo chake pale pale kanisani wakati akimfanyia maombi ya Ibada. Tukio hilo lilitokea kwenye hilo eneo la kanisa. Alikuwepo kanisani hapo mke wa huyu Nuhu Ayoub pamoja akiwa pia na huyu bwana Samwel,” alisema Kamanda Matei.
Aidha Kamanda Matei amewatahadharisha viongozi wote wa dini kuwa makini wanapofanya huduma za maombezi kwa wagonjwa na ikiwezekana waombe msaada wa ulinzi kutoka vyombo vya dola.
“Kwa tukio kama hili, tunawatahadharisha viongozi wengine wa dini wanapofanya kuombea wagonjwa wajaribu kuwa makini. Ikiwezekana kama wanakuwa ni wagonjwa wengi basi wasishindwe kuomba msaada kwenye vyombo vya dola kama vitakuwepo,” alitahadharisha Kamanda Matei.