SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 6 Septemba 2017

T media news

Waziri Mkuu Atoa ONYO Dosari Uaandaji wa Bajeti

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua mifumo miwili ya kielektroniki itakayosaidia kuandaa bajeti kwenye ngazi ya serikali za Mitaa huku akitoa onyo kali kwamba mifumo hiyo isitumike kukwamisha shughuli au utaratibu wa kazi za serikali .

Waziri Majaliwa amezindua mifumo hiyo jana  mjini Dodoma na kusema lengo la mifumo hiyo mipya ni kuongeza uwajibikaji na ufanisi na kamwe isiwe kikwazo katika utoaji wa huduma kwa jamii.

"Napenda kutumia fursa hii kuwafahamisha viongozi na watendaji pamoja na wananchi wote kwamba, lengo la matumizi ya mifumo ya TEHAMA ni kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za serikali na isitumike kukwamisha shughuli au utaratibu wa kazi za serikali. Ni muhimu mifumo hiyo itumike kwa ufasaha ili kuleta tija inayotarajiwa na kila muhusika kwa ahakikishe anailinda, anaitunza na kuitumia mifumo hiyo ili iweze kudumu na kuwa endelevu kwa manufaa ya taifa", alisema Waziri Majaliwa.

Pia Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa mikoa na Halmashauri na vituo vya kutoa huduma za elimu na afya kutoa taarifa ya mapato na matumizi kwa mamlaka zinazohusika kwa wakati.

"Ngazi zote za mamlaka za serikali za mitaa zitoe taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi wanaowahudumia kupitia mikutano, mbao za matangazo, tovuti, vyombo vya habari na njia nyinginezo", alisisitiza Waziri Majaliwa.

Waziri Mkuu alisema kwa sasa serikali haitarajii kuona kituo chochote cha kutoa huduma za elimu na afya kilichopo chini ya Halmashauri kinakuwa na matumizi yasiyozingatia taratibu na kanuni za fedha za umma.

"Hatutarajii kuona viongozi wa mikoa na Halmashauri wakibadilisha matumizi ya fedha bila kuwasiliana na Mamlaka husika. Matumizi ya fedha yafanyike kutegemea chanzo cha fedha kilichopokelewa kwa wakati na kwa mujibu wa bajeti iliyotengwa kwa mwaka husika. 

"Serikali ina matarajio makubwa na mifumo hii, na nitapenda Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Ofisi yangu zipate taarifa zote za mipango, bajeti pamoja na taarifa za fedha zinazopelekwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa wakati na zikiwa katika ubora wa hali ya juu." alisema Waziri Majaliwa

Mifumo iliyozinduliwa jana ni mfumo wa kupanga mipango, kuandaa bajeti na kutolea taarifa za hatua za utekelezaji wa bajeti (Planning, Budgeting and Reporting System- PlanRep) pamoja na mfumo wa kufanya malipo na kutoa taarifa za fedha ambazo zimetumwa kwenye vituo vya kutoa huduma (Facility Financial Accounting and Reporting System-FFARS).