SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 14 Septemba 2017

T media news

Wazawa wanaokosekana VPL msimu huu baada ya kupata deal za nje

Thomas Ng’itu

MSIMU mpya wa 2017/8 ukiwa unaendelea kutimua vumbi, wachezaji wengi ambao walikuwepo katika msimu uliopita wa 2016/7, hawapo katika vilabu vyao baada ya kupata dili za kwenda kusakata kabumbu nje ya Tanzania.

Wachezaji hao wanajumuishwa wachezaji wazawa ambao baada ya kucheza katika ligi Kuu Bara wamefanikiwa kupata timu nje ya nchi kutokana na vipaji vyao kuvishawishi vilabu vya nje na kuamua kuwasali kwa ajili ya kuvisaidia vilabu hivyo.

ShafihDauda.co.tz inakuletea orodha ya wachezaji hao ambao walikuwepo msimu uliopita lakini msimu huu hawapo baada ya kudaka dili hizo.

Rashidi Mandawa

Straika huyu amejiunga na klabu ya BDF inayoshiriki ligi Kuu ya nchini Botswana, alianza kuonekana mzuri tangu akiwa anakichezea kikosi cha Kagera Sugar na kila siku ambavyo zilivyokuwa zinasonga mbele alizidi kuimarika.

Mandawa ameonyesha umahiri katika nafasi ya ushambuliaji, hali ambayo ilikuwa ikimfanya asikae muda mrefu katika vilabu alivyopitia, umahiri wake na upambanaji umemfanya aweze kuushawishi uongozi wa BDF kumwaga fedha kwaajili ya kumchukua.

Mandawa baada ya kuichezea Kagera Sugar, Mwadui na Mtibwa msimu huu amekuwa miongoni mwa wachezaji waliokosekana katika ligi kuu.

SIMON MSUVA

Winga huyu ameonyesha kuwa kwenda nje kuna faida yake, kwani tangu ameenda nje na kurejea katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Botswana, ameonyesha ni mchezaji ambaye ameongezeka vitu katika miguu yake kwani aliweza kuifungia Stars mabao mawili.

Msuva ameondoka nchini akiwa ndiye kinara wa mabao akifungamana na Abdulrahman Mussa kwa mabao 14, lakini msimu huu kukosekana kwake inawezekana ikawa ni fursa kwa wachezaji wengine kushika nafasi hiyo.

ABDI BANDA

Msimu uliopita alikuwa anaitumikia Simba kama beki wa kati lakini akiwa ni mchezaji mwenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya mbili uwanjani, anaweza kutumika kama beki wa kushoto au kiungo wa ukabaji.

Amepata dili nchini Afrika Kusini kukipiga Baroka FC inayoshiriki ligi kuu ya nchini humo, tayari amefanikiwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaopanza kwenye kikosi cha kwanza na alifunga goli lake la kwanza kwenye ligi hiyo wakati Baroka ilipocheza dhidi ya Orlando Pirates na kupata sare ya kufungana 1-1.

Ni mchezaji wa timu ya taifa pia na aliiitwa kwenye mchezo wa hivi karibuni wa kirafiki kati ya Stars na Botswana ukiwa ni mchezo wake wa kwanza tangu ajiungo na Baroka FC

JOHN JEROME

Beki huyu alikuwa anakipiga katika klabu ya Mbeya City lakini msimu huu hayupo tena katika kikosi hicho.

Jerome amepata zali katika klabu ya Real Nakonde inayoshiriki ligi kuu nchi Zambia na amekuwa miongoni mwa wachezaji ambao wamekuwa tegemeo katika kikosi hicho.

Tayari ameshaingia katika orodha ya wachezaji wa Tanzania ambao wanakipiga nje ya Tanzania vilevile anaikosa ligi kuu Bara msimu huu.