SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 2 Septemba 2017

T media news

Watatu watakaocheza kwa mara ya kwanza Stars tangu wawe wa kimataifa

Leo September 2, 2017 timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inacheza mechi ya kirafiki ya kalenda ya FIFA dhidi ya Botswana kwenye uwanja wa Uhuru, Dar.

Kitu cha kuvutia katika mchezo huo ni kuona ongezeko la wachezaji wa Tanzania wanaocheza ligi za nje. kuna wachezaji ambao endapo watapata fursa ya kupangwa, watakuwa wanacheza kwa mara ya kwanza Stars tangu walipotoka kwenda kucheza nje ya nchi.

Abdi Banda 

Kwa sasa anacheza Baroka FC ya Afrika Kusini, ni beki wa kati kijana ambaye hakuna mtanzania ambaye hafahamu juu ya uwezo wake. Amefanikiwa kucheza mechi mbili za kwanza za ligi ya Afrika Kusini (Absa Premiership) akianza kwenye kikosi cha kwanza.

August 22, 2017 alifunga goli lake la kwanza ndani ya Baroka FC wakati walipotoka sare ya 1-1 na Orlando Pirates. Ameitwa mara kadhaa kwenye kikosi cha Stars tangu akiwa Simba, lakini ameitwa kwa mara ya kwanza akiwa mchezaji wa Baroka.

Simon Msuva

Nyota Mwingine ambaye watanzania wengi walikuwa wakipiga kelele aende kutafuta maisha ya soka nje ya Tanzania, akafanikiwa baada ya kusajiliwa na Difaa El Jadid inayoshiriki ligi kuu ya Morocco.

Msuva tangu ajiunge na El Jadid amewasha moto kisawasawa, katika mechi 11 alizocheza amefanikiwa kufunga mabao 9 huu ni mwanzo mzuri kwake.

Na yeye ni kama Banda tu, ameshacheza mechi nyingi akiwa na uzi wa bendera ya Tanzania lakini ameitwa kwa mara ya kwanza tangu awe mchezaji wa nje ya nchini. Watu wanasubiri kuona mambo kutoka kwake endapo atapewa nafasi na kocha wa Stars Salum Mayanga.

Hamisi Abdallah

Huyu ni kiungo wa kati anacheza katika klabu ya Sony Sugar ya Kenya, jina hili ni jina geni masikioni na machoni mwa wengi. Ameitwa kwa mara ya kuongeza nguvu kwenye kikosi cha Mayanga.

Endapo atapewa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha leo huenda watu wengi watatamani kuona kijana atafanya nini alichokuja nacho kutoka Kenya.

Wachezaji wengine wa kimataifa walioitwa Taifa Stars ni nahodha Mbwana Samatta, Farid Mussa na Elias Maguli (hawa wamewahi kucheza na kuonekana mara nyingi tangu wawe wachezaji wa kimataifa)

Morel Ergenes ni kiungo wa pembeni anaecheza Ureno, ameitwa kwenye kikosi cha taifa lakini ameshindwa kuja kwa sababu badhi ya taratibu (za kiusalama) hazikukamilika mapema.