SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 16 Septemba 2017

T media news

Sababu za Polisi kuzuia maombi ya Tundu Lissu

Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) wamesema kuwa hawakubaliani na zuio la kufanya maombi kwa ajili ya Tundu Lissu lililotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kwani shughuli hiyo haihusishi maandamano kama alivyodai.

BAVICHA wameyasema hayo jana wakati wakiongea na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya CHADEMA, Dar es Salaama ambapo wameonyesha kusikitishwa kwao na uamuzi huo.

Katika taarifa ya BAVICHA iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa chama hicho, wamemtaka Kamanda Mambosasa kuisoma tena nakala ya barua yao walioipeleka kuomba kibali, wakisema hawakueleza kwamba kutakuwa na maandamano sababu shughuli hiyo si ya kisiasa.

Hapa chini ni taarifa ya BAVICHA kwenda kwa kamanda hiyo;

Mosi, shughuli yetu ya Jumapili haijapangwa kuhusisha wala haitahusisha maandamano yoyote kama ambavyo SACP Mambosasa ametafsiri. Tumesema wazi katika taarifa yetu kwa jeshi hilo wilayani Kinondoni, kuwa shughuli ambayo tumeiandaa inahusu *MAOMBI* ambayo yatahusisha watu wa imani za dini mbalimbali ambao kimsingi hawawezi kukutana ndani ya nyumba moja ya ibada lakini wote hao wanaweza kukutana sehemu moja, mahali pa wazi na kuomba DUA/SALA kwa utulivu pamoja.

Pili, tunaelewa sheria na taratibu za nchi zinazosimamia mikusanyiko mbalimbali haziwapatii Polisi mamlaka yoyote ya kuzuia mikusanyiko au kutoa kibali cha mikusanyiko, bali sheria na taratibu hizo zimeelekeza wahusika wa shughuli hiyo kutoa taarifa Polisi na kueleza siku, mahali, muda na wahusika wa mkusanyiko husika.

Baada ya kusikia kauli ya SACP Mambosasa, tunatoa wito kama ifuatavyo;

i. Tunamsihi SACP Mambosasa apate nakala ya barua yetu ya taarifa kuhusu shughuli hiyo ambayo tumepeleka mamlaka za kipolisi kama sheria inavyoelekeza, ili aweze kutafakari uzito wa shughuli hiyo ya Maombi ya Kitaifa ya Vijana kisha alinganishe na kauli zake alizotoa leo.

ii. Wakati tukiendelea na maandalizi ya shughuli hiyo ikiwa ni pamoja na taratibu zote za mwisho kufanikisha shughuli hiyo ya *KIIMANI* na si ya kisiasa kama ambavyo SACP Mambosasa anataka kuonesha, tumeitisha kikao maalum cha dharura cha vijana wote wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Viongozi Kitaifa wa Vijana kwa ajili ya hatua za mwisho kufanikisha shughuli hiyo ya kumuombea Lissu ambaye hali yake bado ni mbaya akiendelea kuwa chumba cha uangalizi maalum Hospitali ya Nairobi, nchini Kenya.

Wakati madaktari wanafanya kazi ya kutibu, tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu anayeabudiwa na watu wa madhehebu ya dini mbalimbali, anafanya kazi ya UPONYAJI kupitia *MAOMBI*.

Tunaendelea kuwakaribisha vijana, wanawake, wazee na wananchi wote wenye mapenzi mema na taifa letu na ambao wameguswa na tukio la kinyama na kikatili alilofanyiwa Lissu, katika viwanja vya TP Sinza, Dar es Salaam, kumuombea Mhe. Lissu na taifa kwa ujumla ili liepuke kuandamwa na dhambi ya matendo ya namna hiyo yanayodaiwa kufanywa na watu wasiojulikana ili tukiamini kuwa Mwenyezi Mungu anaweza kujibu kilio cha Watanzania kuwaanika watu hao waovu na kuyafanya majukumu ya polisi ambayo ni kazi ya mikono ya binadamu, kuwa rahisi.

_____________________
Julius Mwita
Katibu Mkuu
BAVICHA Taifa