Ofisa mmoja wa chama cha upinzani cha Union for Peace and Development (UPD), Leopold Habarugira ametekwa na watu wasiojulikana juzi jioni mjini hapa alipokuwa akitembea barabarani na mkewe.
Kwa mujibu wa mkewe, Liberty Nzitonda kiongozi huyo mwenye miaka 54 ambaye ni mweka hazina wa UPD alitekwa na watu wanne, mmoja kati yao akiwa na sare za polisi aliyekuwa na bunduki, wakamweka kwenye gari na kuondoka naye.
“Nina hofu kwa sababu najua kwamba watu wamekuwa wakitekwa hapa nchini kisha miili yao kuonekana baadaye au kupotea kabisa,” Liberty aliliambia shirika la habari la AFP.
Rais wa UPD, Chauvineau Mugwengezo ambaye yuko uhamishoni alisema kutekwa kwa Habarugira “kunafanana na mbinu wanazotumia SNR (Idara ya Usalama wa Taifa)”
Polisi hawakupatikana kuzungumzia tukio hilo.
Habarugira ni mfanyabiashara na mmoja wa wapinzani wachache ambao walikuwa nchini Burundi licha ya mashambulizi dhidi ya wakosoaji wa Serikali. Liberty amesema mumewe aliponea chupuchupu jaribio la kuuawa mwaka 2016.
Rais wa zamani wa chama hicho na msemaji wa UPD aliuawa mwaka 2015. Burundi inakabiliwa na mgogoro kati ya Serikali na wapinzani ambao hutoweka na kuteswa, huku wengi wakilazimika kwenda kuishi uhamishoni.
Ofisa mwingine UPD aliyeuawa katika mazingira ya kutatanisha ni Patrice Gahungu na inadaiwa sababu kubwa ni upinzani wake dhidi ya kusudio la Rais Pierre Nkurunziza kuwania Urais kwa muhula wa tatu kinyume cha Katiba.