Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka na mwenzake kulipa faini ya Sh35 milioni kila mmoja au kutumikia kifungo cha miaka sita jela.
Mbali na Mattaka, mshtakiwa mwingine ni Elisafi Mathew aliyekuwa kaimu ofisa mkuu kitengo cha fedha cha ATCL.
Uamuzi huo umetolewa na Mahakama baada ya upande wa Jamhuri kuthibitisha mashtaka dhidi yao pasipo kuacha shaka.
Akitoa hukumu, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa alimuachia huru William Haji aliyekuwa mkaguzi mkuu wa Hesabu za ndani ATCL, baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka pasipo kuacha shaka dhidi yake.
Mahakama pia imeamuru Mattaka na Mathew kulipa hasara waliyoisababishia ATCL katika ununuzi wa magari chakavu 26 ambayo ni Dola 143,442.75 za Marekani ndani ya mwezi mmoja.
Washtakiwa walitiwa hatiani katika mashtaka sita yaliyokuwa yakiwakabili ya kula njama, matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia hasara Serikali.