SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 3 Septemba 2017

T media news

Mayanga alijihami, Msuva akafunguka

Mwandishi wetu

Licha ya kuwa kocha Salum Mayanga alikuwa kama anajihami katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Botswana,baada ya kucheza mchezo wa kujihami kwa kutumia mfumo wa 4-2-3-1,winga wa Stars Simon Msuva amefunguka na kuonyesha kuwa ni mchezaji mwenye umuhimu katika kikosi hicho.

Katika upande wa ulinzi kipa Aishi Manula ameonesha bado anaendelea kuwa kwenye kiwaango cha juu nchini, baada ya kuendelea kufanya vizuri akiwa katika timu ya Taifa mpaka klabu yake.

Upande wa mabeki kuongezeka kwa Kelvin Yondani, kumefanya kuongeza nguvu kwenye ulinzi kwani waliweza kuelewana na Abdi Banda katika ulinzi wa kati, lakini hata katika beki za pembeni Gadiel Michael na Erasto Nyoni wameonesha kuwa ni mabeki ghali wa pembeni hivi sasa nchini.

Msuva alionekana kuwa katika kiwango cha hali ya juu, hali ambayo iliwafanya viungo wa Stars wakiongozwa na Mzamiru Yassin kutumia upande wa kulia aliokuwa akicheza Msuva kupitisha mashambulizi, na walifanikiwa baada ya kupata mabao mawili kupitia upande huo.

Mzamiru alionekana kuliweza zaidi duara la katikati baada ya kupata wepesi kutoka kwa Himid Mao na Khamis Abdallah ambao walikuwa wakikaba kwa pamoja, njia ambayo Kocha Salum Mayanga alionekana kufanikiwa katika upande wa katikati.

Katika upande wa ushambuliaji, Mayanga alimsimamisha Mbwana Samatta peke yake hali ambayo ilimfanya mchezaji huyo kushindwa kutamba mbele ya mabeki wa Botswana ambao muda wote walikuwa wakimkamia mchezaji huyo anayekipiga katika klabu ya Genk nchini Ubelgiji.

Katika kipindi cha pili Mayanga alifanya mabadiliko ya kwa kumtoa Shiza Ramadhan na nafasi yake kuchukuliwa na Farid Mussa ambaye aliingia lakini hakuwa katika kiwango chake cha siku zote, mabadiliko ya Khamis Abdallah na kuingia Said Ndemla kumefanya safu ya kiungo kuongeza spidi baada ya awali Himid na Khamis wote kucheza kama viungo wakabaji hali ambayo ilifanya timu isisogee mbele kwa kasi.

Kuongezeka kwa Emmanuel Martin na Maguli napo kuliongeza nguvu, hasa katika upande wa ushambuliaji kwa sabbau Maguli alivyoingia licha ya kucheza dakika chache alikuwa akipambana na mabeki wa Botwasana kwa kutumia nguvu zake, tofauti na ambavyo Samatta alivyoanza lakini hata hivyo uwepo wake ulifanya mabeki wa Botswana wamgeukie yeye na kusahau wengine na hali hiyo ilimfanya Msuva awe huru.