SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 12 Septemba 2017

T media news

Mara paap! Champions League hii hapa

Group A.

Ni mchezo wa 5 kwa Manchester United na Fc Basel kukutana katika champions league lakini katika mara 4 zilizopita hakukuwa na mbabe kwani kila mmoja alishinda mara moja huku wakisuluhu mara 2 na mchezo wa leo pale Old Trafford unaweza kuamua yupi mbabe kati ya wawili hao.


Benfica wakiongozwa na golikipa mkongwe Julio Cesar watakabiliana na CSKA Moscow, kundi hili ukiliangalia kwa makini unaweza kugundua timu zote nne zina nafasi kubwa kusonga mbele kwani wote wana rekodi za kufungana.

Group B
Allianz Arena uwanja wa nyumbani wa Bayern Munich wataanza kwa kuikaribisha Anderchelt toka Ubelgiji, Carlo Ancelloti ana kibarua kigumu kurudisha heshima ya Bayern Munich katika michuano hii na mchezo huu wa kwanza ushindi tu ndio kinachotakiwa.

Matajiri PSG ambao kwa sasa safu yao ya ushambuliaji inaonekana ni tishio kubwa duniani watawafuata Celtic, sio mchezo mrahisi kwa PSG kwani Celtic ni wagumu sana na kama ilivyo PSG wana safu nzuri ya ushambuliaji, unaweza kuwa mchezo wa kufungana kwa kila upande.


Group C

Chelsea watakuwa darajani, wakishuhudiwa wakirejea katika Champions League na safari hii wanakutana na timu ambayo hawajawahi kukutana nayo na wala haijawahi kushiriki Champions League Fc Qarabag, klabu hii ya Azerbijian kama ilivyo kwa Rb Leizpg ya Ujerumani hii ni mara yao ya kwanza kucheza Champions League.


Athletico Madrid nao ambao wanaonekana kuwa na mkosi na michuano hii, leo watasafiri kwenda Italia kuwakabili As Roma, Athletico wamekuwa na rekodi nzuri wanapoanza mashindano haya na mwishoni huwa wanapoteza na leo pia wana nafasi kuibuka na alama hata moja katika dimba la Stadio Olimpico.

Group D.

Paulo Dyabala amefunga mara 4 katika michezo 7 msimu huu lakini kuondoka kwa Bonucci kunawafanya Juventus kuwa hatarini sana kwani eneo lao la ulinzi linaonekana halijakaa vizuri na hii inaweza kuwapa mwanya Luis Suarez, Osmane Dembele na Lioneil Messi kuwatia Juventus majaribuni.


Mchezo huu unasubiriwa kwa hamu na watazamaji wengi kwani unatukumbusha msimu uliopita Barca walivyoondolewa na Juve katika michuano hii na safari hii wanakutana mapemaa, inaweza kuipa nafasi Barcelona kulipiza kisasi au Juventus kuendeleza utemi.

Olympiacos wenyewe watakuwa kwenye dimba lao la nyumbani la Karaiskaki Stadium kuwakaribisha Sporting Cp, hizi ni timu ambazo hazipewi nafasi kabisa kufudhu katika kundi hili kutokana na vigogo waliopo.