SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 1 Septemba 2017

T media news

Bendera za vyama vya siasa zapigwa marufuku barabarani

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa amepiga marufuku upeperushaji wa bendera za vyama vya siasa kandokando mwa hifadhi ya barabara.

Galawa alitoa amri hiyo juzi katika kikao cha wadau wa afya kilichofanyika Vwawa wilayani Mbozi na kusisitiza shughuli zote zinazofanyika katika hifadhi ya barabara kuu ya Songwe-Zambia zikiwamo bendera za vyama zinazopeperushwa eneo hilo ziondolewe ili kuacha maeneo hayo safi.

“Kuanzia leo (juzi) bendera zote za vyama vya siasa zifungwe na kupeperushwa kwenye ofisi za chama husika,” alisema Galawa

Kuhusu uchafu unaozagaa kandokando ya barabara hiyo, Galawa aliwaagiza maofisa wa afya kuwakumbusha abiria kutotupa taka wawapo safarini bali watumie vyombo vya kukusanyia taka vinavyotumika ndani ya magari.

Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Mbozi, James Mbasha alisema kuwa chama chao hakijapata taarifa hiyo huku akieleza kwamba bendera hizo zina wenyewe walioziweka maeneo hayo hivyo ni vyema wahusika wakatafutwa ili waulizwe.

Aidha kiongozi huyo alisema mtendaji yeyote atakayeziondoa bendera hizo watamshtaki mahakamani kwani zipo kwa mujibu wa sheria za nchini.

Kwa upande wa Katibu wa CCM Wilaya ya Mbozi, Rehema Nzyunye alisema kwamba hawajapata taarifa hiyo hivyo hawawezi kuizungumzia.

Chanzo: MWANANCHI