Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema hatakubali kuteuliwa na Rais John Magufuli kushika nafasi yoyote, kwa sababu kukubali kitamnyima fursa ya kujenga Chama chake ili kiwe tayari kushinda uchaguzi na kushika dola.
Mbunge huyo wa Kigoma Mjini, ambaye chama chake kimeshatoa viongozi wawili walioteuliwa kushika nafasi za juu Serikalini, amesema ikitokea Rais Magufuli akamteua, atamshukuru na kukataa uteuzi huo.
Zitto alisema hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi jijini Mwanza mwishoni mwa wiki, alipokuwa akijibu swali kuhusu uteuzi baada ya Rais Magufuli kumteua mwenyekiti wa ACT-Wazalendo "Anna Mghwira kuwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, na mshauri wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Mghwira alivuliwa wadhifa wake, wakati Profesa Kitila alijivua nafasi zote katika chama.
Lakini Zitto hafikirii kufuata mkondo huo.
"Sitakubali uteuzi kwa sababu jukumu langu na viongozi wengine wa ACT Wazalendo ni kukijenga chama ili kipate ushawishi na kuungwa mkono na umma na hatimaye kushika dola", alisema Zitto.
"Kukubali uteuzi utakaoniondoa na kuniweka kando kwenye jukumu na malengo hayo ni kufifisha matumaini ya maelfu ya wana-ACT Wazalendo".
Kauli hiyo inakuja katikati ya maneno na ubashiri kuwa Zitto, ambaye ana shahada ya uzamili katika masuala ya sheria na biashara, anaweza kuteuliwa kujaza nafasi iliyo wazi kwa muda mrefu baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo ya Waziri wa Nishati na Madini.
Akijibu swali kwanini chama chake kiliridhia uteuzi wa Profesa Mkumbo na Mghwira, Zitto alikuwa na sababu tofauti.
"Kwanza, kabla ya uteuzi na hata baada ya uteuzi Profesa Mkumbo ni mtumishi wa umma ndiyo maana uteuzi wake haukushtua", alisema Zitto.
"Mama Mghwira alikuwa ni mwanasiasa kwa nafasi yake ya uenyekiti wa Taifa, ndiyo maana tulimwondoa ili kumpa fursa ya kumtumikia Serikali.
Chanzo: Mwananchi