Wapendanao ndiyo wapatanao! ndivyo walivyosikika baadhi ya mashabiki wa staa wa sinema za Kibongo, Wema Isaac Sepetu na Idris Sultan ambao penzi lao lilivunjika yapata mwaka mmoja uliopita, baada ya kuoneshana mahaba ya kufa mtu na kufufua upya penzi lao.
TUJIUNGE MLIMANI CITY
Mbele ya Ijumaa Wikienda, Wema na Idris walionesha hadharani kuwa penzi lao bado lipo gado na ndiyo kwanza kama linaanza, wakati wa uzinduzi wa sinema mpya ya bishosti huyo inayokwenda kwa jina la Heaven Sent kwenye Ukumbi wa Cinemax, Mlimani City jijini Dar, usiku wa kuamkia jana. Awali, kulikuwa na ukimya fulani, lakini ghafla ukumbi huo ulilipuka kwa shangwe na mshangao baada ya kumuona Wema akiingia na Idris huku wakiwa wameshikana mikono kama ‘bibi na bwana’. Kuna wakati Idris alimkamatia Wema kiuno hadi mama wa bidada huyo, Mariam Sepetu akawa anawashangaa kama vile hakutarajia kuona mahaba niue ya wawili hao.
WEMA ABANWA Wakati wa kuitazama (premier) sinema hiyo, bado Wema aliendelea kuwa beneti na Idris ambapo kwa pamoja waliwakaribisha waalikwa kuitazama sehemu ya sinema hiyo kisha kumkaribisha yeyote mwenye maoni juu ya ‘mzigo’ huo mpya ulioingia sokoni rasmi. “Ninaamini kila mmoja ameona uwezo wangu niliopewa na Mungu kwa kuiangalia filamu yangu hii ya Heaven Sent, ndani ya filamu hii unaweza kuona vizuri mimi ni msanii au naleta longolongo,” Wema aliliambia Ijumaa Wikienda na kuongeza:
MILIONI 40 ZATEKETEA
“Heaven Sent imegharimu shilingi milioni 40 za utengenezaji wake hivyo unaweza kuona ni kwa kiasa gani nipo ‘serious’ na kazi yangu. Cha msingi kama mtu ni shabiki wangu wa ukweli, awahi kupata nakala yake kwani kuanzia wikiendi hii (iliyopita) filamu yangu ya Heaven Sent ipo sokoni.”
WEMA ANG’ATA VIDOLE
Hata hivyo, Ijumaa Wikienda lilipomtaka Wema kuweka bayana kama ndiyo amerudisha majeshi rasmi kwa Idris, staa huyo aliishia kung’ata vidole, kucheka na kusema kuwa ataweka mambo hadharani hivi karibuni, lakini kwa pale ukumbini alifika kwa shughuli maalum ya uzinduzi huo uliohudhuriwa na mastaa kibao akiwemo shosti yake ambaye siku hizi hawapo karibu, Aunt Ezekiel.
IDRIS: WEMA SIYO KIPORO
Kwa upande wake, Idris alipoulizwa kama Wema ndiyo mtarajiwa wake au vinginevyo, alisema kuwa, kwa usiku huo aliomba amsindikize tu kwenye uzinduzi wa filamu hiyo, lakini akawa anasisitiza kuwa Wema si kiporo. “Mimi ndiye nimemuomba kuwa naye, nilipomfuata, kwa bahati nzuri sikumkuta na mwanaume, lakini kwani ukiweka chakula kwenye friji na ukataka kukila unafanyaje? Si unakila? “Lakini sijasema Wema ni kiporo, Wema siyo kiporo. Kwani mke huwa anaachwa? Mke haachwi, nadhani umenielewa,” alisema Idris huku akiangua kilio na kudai kuwa ‘love bite’ aliyokuwa nayo shingoni ilitokana na kung’atwa na mbu!!”
MAMA WEMA AFUMBA MACHO
Hata hivyo, Wakati wawili hao wakiwa kwenye pozi za kimahaba, mama Wema alionekana akifumba macho baada ya kuwapiga chabo kwa mara nyingine na kushuhudia wakiwa wamegandana kama ruba.
WATIMUA PAMOJA
Hadi shughuli hiyo inamalizika, wawili hao waliendelea ‘kupeana mambo matamumatamu’ ambapo Ijumaa Wikienda liliwapiga chabo wakitimua kwenye ndinga, lakini haikufahamika kama walikwenda ‘kumbonji’ kwa Wema au kwa Idris.