Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Cuba, Gladys Bejarano na kumhakikishia ufunguzi wa ofi si za ubalozi wa Tanzania nchini humo.
Amesema Tanzania inayatambua na kuyathamini mahusiano mazuri ya kidiplomasia, kisiasa, kiuchumi, kielimu, kiafya na kiutamaduni kati yake na Cuba, hivyo inatarajia kufungua ubalozi nchini humo ili kurahisisha utendaji wa kazi za kibalozi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa alikutana na Bejarano juzi jioni wakati alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi nchini Cuba. Malengo ya ziara yalikuwa ni kuimarisha na kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
“Tunatambua uhusiano mzuri uliopo kati Tanzania na Cuba, ambao ulikuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hivyo lazima tufungue ofisi za ubalozi na tutamleta balozi wetu hapa,” alieleza Majaliwa.
Pia Waziri Mkuu aliishukuru Serikali ya Cuba kwa ujenzi wa kiwanda cha dawa za kuulia vijidudu vya malaria pamoja na ufadhili wa masomo ya udaktari, inaoutoa kwa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma katika vyuo mbalimbali nchini humo.
Aliiomba serikali hiyo iendelee kutoa ufadhili wa masomo kwa madaktari hao hadi ngazi ya Shahada ya Uzamili kwa sababu Serikali ya Tanzania inawahitaji madaktari bingwa wengi kwani walioko nchini ni wachache.
Kwa upande wake, Bejarano alimshukuru Waziri Mkuu kwa kufanya ziara nchini Cuba na alimhakikishia kwamba uhusiano wa serikali yake na Serikali ya Tanzania utaendelea kuimarishwa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Alisema Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, inafanya jitihada kubwa za kuhakikisha uchumi wake unakua kwa kasi jambo ambalo ni tofauti na mataifa mengine.
Makamu huyo wa Rais alisema Serikali ya Cuba itaendelea kushirikiana na Tanzania katika uboreshaji wa sekta za afya, utamaduni, kilimo, uchumi na elimu. Kuhusu ombi la kuongeza ufadhili wa shahada ya uzamili kwa madaktari, alisema amelip