SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 2 Agosti 2017

T media news

Utamu wa pesa za usajili huenda ukamfukuzisha kazi Guardiola mapema kabla ya msimu kumalizika

Na Salym Juma, Arusha

Pep Guardiola ni kocha anayesifika kwa mbinu za kipekee ambazo zilianza kumtambulisha pale Camp Nou tangu mwaka 2008. Dunia ilinyoosha mikono juu pale Pep alipoiongoza Barcelona kutwaa kila taji kwenye michuano iliyoshiriki. Akiwa Barcelona, sehemu ambayo alicheza na kufundisha kwa mafanikio Pep alijijengea jina hasa kwa staili yake ya uchezaji ya kupiga pasi maarufu kama ‘Tik tak’. Guardiola hakuwahi kufanya vibaya akiwa na Barcelona.

Vikombe vitatu mfululizo vya La liga tangu 2008 hadi 2011 vilitosha kuwafanya Barcelona kutawala soka la Hispania huku Mabingwa wa Ulaya Real Madrid wakibaki washiriki katika michuano mbalimbali nchini Hispania. Copa del Rey ni Kombe kongwe nchini Hispania kama ilivyo FA nchini Uingereza. Guardiola alifanikiwa kuchukua jombe hili mara mbili. Katika misimu minne aliyodumu pale Camp Nou, Pep alifanikiwa kutengeneza ‘Brand’ yake ambayo inadumu hadi leo.

Baada ya kustaafu kila timu ilikuwa na shauku ya kunasa saini ya Pep. Vilabu vingi vilitamani kumpata Pep kwa lengo la kuweza kutwaa ubingwa wa Ulaya wakiwa na Guardiola. Vikombe viwili vya Ulaya alivyotwaa chini ya Barcelona vilitosha kumpa thamani kiungo huyu wa zamani ambaye amecheza kwa mafanikio pale Camp Nou kabla ya kutimkia Italia, Mexico na Uarabuni kwenda kumalizia karia yake ya mpira wa miguu.

Baada ya kuiongoza Barca kushinda kwa 76.32% katika misimu 4, hatimaye mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich walifanikiwa kunasa saini ya fundi huyu ambaye amekuwa akimtesa Mourinho mara kibao. Akiwa Ujerumani, Pep alifanya vizuri nyumbani ila ‘target’ ya Wajerumani haikuwa kushinda taji la Bundesliga pekee bali kubeba ndoo ya UEFA. Kwa misimu mitatu mfululizo nchini Ujerumani, Pep alifanikiwa kutwaa taji la Bundesliga mara zote.

Kutokana na rekodi zake nzuri, Waarabu wa Manchester City walifanikiwa kumsaini Guardiola February 1, 2016 kwa mkataba wa miaka mitatu. Wanasoka wengi walifurahi kumuona Pep katika ligi ya Uingereza kwaniwaliamini hapa ndipo sehemu sahihi pa kupima ubora wa Pep kama kocha bora. Ligi ya Uingereza iliongezeka mvuto baada ya Pep kutia maguu katika jiji la Manchester, sehemu ambayo hasimu wake wa jadi Jose Mourinho yupo.

Msimu wake wa kwanza pale Etihad hakufanya vizuri licha ya kushinda mechi 10 za mwanzo wa ligi na kumfanya kuongoza ligi kwa kishindo. Kipigo cha 2–0 dhidi ya Tottenham Hotspur kilianzisha msukosuko kwa Guardiola katika maisha yake ya ukocha. Man City ilipata wakati mgumu chini ya Pep hasa baada ya kucheza michezo 6 mfululizo bila kupata ushindi. Guardiola alikaririwa akisema hajawahi kupitia wakati mgumu katika maisha yake ya ukocha kama wakati huo.

Kutokufanya vyema kwenye michuano ya ligi kuu, FA na EFL kulimfanya Pep abakize matumaini yake kwenye michuano ya Ulaya, michuano ambayo amekuwa na uzoefu nayo kwa muda mrefu. Kupangwa na Barcelona katika kundi la C kwenye michuano ya Ulaya kulimfanya Pep kuumia kichwa ila alimaliza na alama 6 nyuma ya Barca iliyokuwa na alama 15. Baadae Monaco walimsambaratisha Pepkatika hatua iliyofuata na kuzima ndoto za Guardiola kuambulia angalau kikombe kimoja.

Kwa msimu uliomalizika Pep aliiongoza City kushinda kwa 60.5%, wastani ambao ni mdogo tangu aanze kufundisha Soka. Pep alizungumza mara kadhaa hadharani huku akijitetea kuwa wachezaji wenye umri mkubwa kikosini ndio chachu ya yeye kufanya vibayamsimu uliomalizika. Baada ya ligi kumalizika, Guardiola alifanya mabadiliko makubwa katika kikosi cha City. Wachezaji wengi wenye umri mkubwa na viwango vya kawaida walitoswa na damu changa kuingia.

Mfaransa Gaël Clichy, Willy Caballero,Winga Jesús Navas, Bacary Sagna, Pablo Zabaleta, Nolito na Aleksandar Kolarov ni baadhi yamajembe ambayo yalifungashiwa virago na Guardiola mapema sana baada ya msimu kumalizika. Kuondoka kwa wachezaji hawa kuliwapa fursa vijana wadogo wenye kasi kusajiliwa Etihad. Pep alitumia pesa nyingi pia kuwasajili baadhi ya wachezaji pindi alipotangazwa kujiunga na City kutoka Munich.

Benjamin Mendy, Danilo, Kyle Walker, Bernardo Silva na mlinda mlango Ederson ni miongoni mwa wachezaji ambao huenda wakamfukuzisha kazi Pep Guardiola kabla ya msimu wa 2017-18 kumalizika. Inawezekana usinielewe ninachomaanisha ila lugha nyepesi isiyohitaji maelezo ya ziada ni kwamba Pesa nyingi alizotumia Pep zinamfanya apate mafanikio kwa lazima na endapo itakuwa kinyume na hapo naamini Waarabu hawatamtazama mara Mbili.

Douglas Luiz, Eric García na Uriel Antuna wamekamilisha usajili wa City hadi sasa licha ya dirisha kuendelea kuwa wazi. Hadi sasa Guardiola ametumia Zaidi ya £200 million katika usajili hasa katika kuijenga idara ya ulinzi ambayo ilionekana kupwaya msimu uliopita. Guardiola alishatumia kiasi kikubwa cha Pesa majira yaliyopita kwa kuwasajili Gabriel Jesus, Leroy Sané, İlkay Gündoğan, John Stones na Claudio Bravo. Naweza kusema hii ni kufuru ya Pep kwenye usajili.

Nikihitimisha kwa maneno machache, naweza kusema ule msemo wa Mwarabu sio Mtu mzuri unaweza kumkuta Pep msimu ujao endapo mambo yatamwendea kombo kwani naamini pesa zilizotumika zitahitaji mafanikio hasa katika makombe mawili, EPL na UEFA Champion League. Vikombe kama FA na EFL vinaweza kuwa vya ziada kwa Waarabu wa City. Pep atakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Mourinho, Conte, Pochetino, Wenger na Klop.