SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 7 Agosti 2017

T media news

Rais Magufuli atangaza msamaha wa kodi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 07 Agosti, 2017 amemaliza ziara ya kikazi ya siku 5 katika Mkoa wa Tanga kwa kuzungumza na wananchi wa Wilaya za Korogwe na Handeni pamoja na kufungua kituo cha mabasi cha Korogwe.

Kituo hicho chenye vyumba vya maduka 122 kimejengwa na Serikali ya Tanzania kwa gharama ya Shilingi Bilioni 4.023, na ni kati ya vituo vya mabasi 11 vinavyojengwa katika miji mbalimbali hapa nchini kwa gharama ya takribani Shilingi Bilioni 360.

Akizungumza na wananchi wa Korogwe muda mfupi kabla ya kufungua kituo hicho Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wakandarasi waliojenga kituo hicho kwa kazi nzuri waliyoifanya na ameonya kuwa Serikali haitamvumilia mkandarasi yeyote atakayechelewesha ama kujenga mradi wa Serikali chini ya kiwango.

Mhe. Rais Magufuli amepokea ombi la Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo kusamehewa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika mradi huo na ameagiza miradi yote inayotekelezwa na Serikali ama kwa fedha za ufadhili isitozwe VAT.

“Haiwezekani miradi hii ni ya Serikali, au inatekelezwa kwa fedha za msaada ama mkopo nafuu halafu sisi wenyewe Serikali tunatoza VAT, kama kuna sheria tuzibadilishe, lakini kama kuna vifaa vimezuiwa kwa ajili ya VAT viachiwe ili miradi iendelee” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amepokea kero ya uhaba wa maji na mgogoro wa kiwanda cha chai cha Bumbuli na ameahidi kuzifanyia kazi.

Wilayani Handeni Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Kibaoni na ametoa wiki 2 kwa wakandarasi waliokuwa wakijenga mradi wa mabwawa 3 ya maji kwa ajili ya Miji ya Manga, Mkata na Kwandugwa kurejea na kuendelea na kazi ya ujenzi wa mradi, vinginevyo wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Hela ya Serikali ninayoiongoza haiwezi kupotea bure, mradi huu ulitengewa Shilingi Bilioni 4.1, hawa wakandarasi walishalipwa Shilingi Bilioni 2.8 na ninafahamu kuwa hawapo kazini na mradi umesimama, nataka ndani ya wiki mbili wawe wamerudi na kuendelea na kazi, wasipofanya hivyo wakamatwe” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Pamoja na mradi huo Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Handeni kuwa Serikali imejipanga kutumia Shilingi Bilioni 200 kumaliza tatizo la maji katika Mji huo na vijiji vitakavyopitiwa na bomba la maji kutoka mto Pangani.

Mhe. Dkt. Magufuli pia amepokea kilio cha wananchi wa Handeni waliodai kuondolewa kikatili katika maeneo yao ya makazi na mashamba ili kumpisha mwekezaji wa uchimbaji wa madini na amewataka kutulia wakati anafanyia kazi kilio hicho.

Akiwa njiani Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa katika vijiji vya Msima, Kwachaga na Manga ambako amesikiliza kero za wananchi juu ya ukosefu wa madaktari, uhaba wa maji na ukosefu wa umeme katika baadhi ya vijiji na amewahakikishia kuwa Serikali itatatua kero hizo kwa kuwa mipango ipo.

Katika Kata ya Kwachuma, Mhe. Rais Magufuli ameagiza kuondolewa kwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Mazingara baada ya wananchi na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bw. Godwin Gondwe kudai amekuwa akitoa uamuzi usiotoa haki kwa wakulima pale wanapolalamikia mashamba yao ya mazao kuvamiwa na mifugo.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa Bunju “B” katika Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam ambapo wafanyabiashara wadogo wamelalamikia kuondoshwa katika maeneo yao ya biashara, na Mhe. Rais amesitisha zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara hao kwa siku 4 na ameahidi kumtuma Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul Makonda na wataalamu wengine kuchunguza malalamiko hayo ili kupata ufumbuzi.

Mhe. Rais Magufuli amerejea Jijini Dar es Salaam.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

07 Agosti, 2017