SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 7 Agosti 2017

T media news

Mambo 10 yasiyofanywa na watu imara kiakili

Uimara wa akili hauonekani kwenye mambo unayoyafanya. Mara nyingi unaonekana kwenye mambo ambayo hutaki kuyafanya. Kuimarisha akili yako inakuhitaji uwe na uwezo wa kutawala au kudhibiti fikra, tabia na hisia.

Yafuatayo ni mambo ambayo watu wenye akili imara hawayafanyi au wanajizuia kuyafanya.

1. Hawapotezi muda kusikitika kwa makosa waliyofanya

Kusikitika kutokana na makosa uliyofanya inasababisha usiwe sawa. Kutumia muda wako ukisikitika kwa makosa yako kunakuzuia kufurahia maisha, inakupotezea muda bila sababau, inakuletea hisia hasi na ina madhara makubwa kwenye uhusiano wako na watu wengine.

Jambo la muhimu ni angalau kuanza kusifu mambo mazuri yanayokuzunguka, na utajikuta ukifurahia neema ulizo nazo pia. Lengo kubwa la kufanya hivi ni kuondoa mawazo ya kujiona huna thamani na kuwa na mawazo ya shukrani.

2. Hawakubali kupoteza nguvu waliyonayo

Watu wengi wanajikuta wakijionesha kuwa hawana nguvu au uwezo wa kufanya lolote wanaposhindwa kuwawekea watu wengine mipaka ya kimwili na kihisia. Unatakiwa uwe na uwezo wa kujitetea na kuonesha mipaka waziwazi kama ikikulazimu. Kama watu wengine wanaweza kuamua ufanye nini, wao ndio watakuwa na nguvu ya kuamua kiwango cha maendeleo yako pamoja na utakuwa unajiona una thamani kiasi gani. Ni muhimu kuhakikisha kuwa unajiwekea malengo na ufanye kazi kuyatimiza.

Watu waliokumbwa na matatizo makubwa utotoni mwao, kama kubakwa, kufiwa na wazazi au kunyanyaswa wanakuwa kwenye hatari ya kujiona hawana thamani maisha yao yote. Lakini wengine waliopata matatizo kama hayo hujikuta wakifikia uamuzi wa kuchagua wanataka kutambuliwa namna gani ukubwani mwao.

3. Hawakimbii mabadiliko

Kufanya mabadiliko maishani yaweza ikawa ni jambo la kuogopesha. Iwe ni kubadili kazi, uhusiano au jambo jingine lolote kubwa maishani mwako. Pamoja na kuogopesha kwake, kukimbia mabadiliko kunakusababisha usipate fursa za maendeleo. Unapozidi kusubiri, unazidi kuchelewa. Watu wengine watakupita.

4. Hawajihusishi na mambo wasiyoweza kuyadhibiti

Ni hisia nzuri sana ukijua kila kitu kipo sawa chini ya usimamizi wako, lakini kufikiri kwamba tuna uwezo wa kudhibiti kila kitu muda wote inaweza kutuweka matatizoni.

Badala ya kufikiria jinsi ya kujiondolea wasiwasi, fikiria jinsi ya kuyamudu mazingira yako. Kubadili fikra zako kutoka kwenye mambo usiyoweza kuyadhibiti itakuongezea furaha, kukupunguzia msongo wa mawazo, kuboresha uhusiano wako na wengine, fursa mpya na mafanikio zaidi.

5. Hawana wasiwasi juu ya kumfurahisha kila mtu

Mara nyingi tunapima kukubalika kwetu kwa kuangalia watu wengine wanatungumziaje, jambo ambalo ni kinyume kabisa cha uimara wa akili. Unakuwa unajaribu kuwaridhisha watu kuna athari kadhaa: kupoteza muda; kudanganywa kirahisi; ni sawa watu kukukasirikia na huwezi kumrithisha kila mtu.

Kuacha fikra zako za kutaka kumridhisha kila mtu kutafanya uwe imara zaidi na mwenye kujiamini.

6. Hawaogopi kujaribu mambo mapya

Mara nyingi watu wanaogopa kujifunza au kufanya mambo mapya, haijalishi kama yanahusu fedha, mwili, hisia, kijamii au kibiashara. Lakini yote hii ni kutokana na kutojua. Kukosa elimu ya jinsi ya kupanga namna bora ya kufanya jambo kwa umakini kunasababisha woga.

Ili uweze kuepuka hasara zitokanazo na kufanya jambo jipya, majibu yako kwenye maswali yafuatayo yanaweza kukuongoza:

—Gharama inayotarajiwa ni ipi?

—Faida zitazopatikanani zipi?

—Jambo hili litasaidia vipi niweze kufanikisha lengo langu?

—Njia mbadala ni ipi?

—Jambo gani zuri nitalipata kama kila ninachotarajia kitafanikiwa?

—Jambo gani baya zaidi litatokea kama nikishindwa kabisa, na nitaweza kulizuiz vipi?

—Kama jambo baya kabisa litatokea kwenye hili, litakuwa baya kiasi gani?

—Uamuzi nitaoufanya sasa nitauona vipi baada ya miaka mitano?

7. Hawajali yaliyopita

Yaliyopita yamepita. Hakuna namna ya kuweza kurudi nyuma na kuyabadilisha na kuendelea kuyang’ang’ania yaliyopita ya kuna matatizo makubwa, utashindwa kufurahia wakati wa sasa wala kuweka mipango kwa ajili ya maisha yako ya baadaye. Haikusaidii kutatua chochote na sanasana itakuletea msongo wa mawazo.

Pamoja na kusema haya, kunaweka kukawa na faida ya kufikiria kuhusu yaliyopita. Kufikiria masomo uliyoyapata kutokana na hasara au mambo uliyoshindwa kuyafanya na kufikiria jinsi ya kufanya hali kama hiyo ikitokea tena.

8. Hawarudii makosa waliyofanya nyuma

Kufikiria kuhusu makosa uliyowahi kuyafanya kunasaidia kutoyarudia tena. Ni muhimu kujifunza kwa makosa uliyoyafanya, ujue nini ungeweza kukifanya vizuri zaidi na nini hasa utakachofanya baadae.

Watu walio imara kiakili wanakubali majukumu yanayotokana na makosa waliyofanya na kubuni njia bora, kuandaa mkakati (mara nyingine kimaandishi) wa kuepuka kurudia makosa hayo wakati mwingine.

9. Hawana kinyongo na mafanikio ya wengine

Kinyongo ni kama hasira ambayo haijatoka. Kuwaza sana kuhusu maendeleo ya mtu mwengine hakutasababisha na wewe ufanikiwe kwakuwa inakutoa katika kuwaza jinsi ya kutimiza mipango yako.

Hata ukipata mafanikio, unaweza usiridhike kama utakuwa unawaza kuhusu watu wengine muda wote. Pia kuna hatari ya kujikuta unasahau kuendeleza vipaji ulivyonavyo na kuacha unayoyaamini na mwisho kujikuta unavunja uhusiano.

10. Hawakati tamaa baada ya kushindwa mara moja

Mafanikio hayapatikani kwa haraka na vikwazo ni lazima utakumbana navyo katika kutafuta maendeleo. Kufikiria kwamba vikwazo vinamaanisha kwamba huna uwezo wa kutosha kufanya jambo fulani si moja ya tabia za watu wenye akili imara. Ukiweza kurekebisha makosa yaliyotokana na vikwazo vya awali, utakuwa imara zaidi ulivyokuwa awali.