SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 9 Agosti 2017

T media news

Rais Magufuli ataka VAT iondolewe Kwenye Miradi ya Ufadhili


RAIS John Magufuli ameziagiza wizara za Fedha na Mipango na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tamisemi kuandaa mapendekezo na kupeleka bungeni mwaka huu marekebisho ya sheria yanayotaka kulipwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa miradi inayopata ufadhili kutoka kwa wadau wa maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia.

Ametoa agizo hilo wakati akihutubia wananchi wa Korogwe waliohudhuria ufunguzi wa stendi mpya ya kisasa ya mabasi iliyogharibu Sh bilioni nne eneo la Kilole. Dk Magufuli alisema utaratibu huo unafanya serikali kulipa VAT kwa serikali yenyewe jambo ambalo si sahihi kwa kuwa fedha hizo zingetumika kufanya shughuli nyingine za maendeleo.

Alitoa agizo hilo baada ya Naibu Waziri Tamisemi, Selemani Jaffo kueleza kuwa ipo changamoto ya kisheria inayokabili miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali kutakiwa kulipa VAT na kusababisha serikali kulipa fedha za ziada Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa sababu mikopo na ruzuku kutoka kwa wafadhili hazitengi malipo ya kodi.

“Nawaagiza mawaziri wa wizara zote mbili kuandaa marekebisho ya sheria hii ambayo ilipitishwa mwaka 2015 ili mwezi Septemba iweze kurekebishwa bungeni... tunahitaji fedha, lakini sio kwa kila kitu tutozwe VAT hiyo ni kujichelewesha hayo mambo ni ya ovyo lazima tuyaache,” alieleza Dk Magufuli.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amemuomba rais kushughulikia mgogoro wa kiwanda cha kusindika chai cha Mponde wilayani Lushoto ambao umechukua muda mrefu na kusababisha wakulima wa Jimbo la Bumbuli wilayani humo kushindwa kujiendeleza kiuchumi. Stendi iliyojengwa mjini Korogwe ni miongoni mwa mradi 11 inayojengwa na kusimamiwa na Tamisemi kwa ufadhili wa Benki ya Dunia katika baadhi ya halmashauri nchini.