Wakati Chama cha Wananchi (CUF) kilipokuwa kwenye misukosuko baada ya kupokea barua ya kujiuzulu kwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, dhamana ya uimara na amani ya chama hicho ilikuwa chini ya Mwenyekiti wa muda wa chama hicho Julius Mtatiro ambaye aliteuliwa na Baraza la Uongozi la chama hicho ambapo alikuwa na dhamana ya kuhakikisha kuwa chama kinaendeshwa kwa mafanikio. Yeye ndiye alipaswa kutoa dira ya chama kielekee wapi.
Kwa bahati mbaya sana, chama kilipopigwa na mawimbi, Mtatiro (bila shaka baada ya kushauriana na Katibu Mkuu, Maalim Seif Shariff akatoa muongozo ambao kwa kiasi kikubwa umewapotosha wana-CUF nchi nzima kiasi kuwa leo hii wanajikuta katika sintofahamu kubwa ambayo inatishia muelekeo wa chama hicho.
Wakati Profesa Lipumba alipotangaza kufuta barua yake ya kujiuzulu na kuamua kurejea katika nafasi yake kama Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Mtatiro alikuwa mmoja wa viongozi wa awali kabisa wa CUF kuonesha dharau kwa Profesa Lipumba. Mbaya zaidi hakuonesha dharau yeye binafsi tu, kauli zake ziliwaelekeza wanachama wengine wa CUF wampuuze Profesa Lipumba na kundi lake. Hili lilikuwa kosa kubwa sana ambalo Mtatiro anapaswa kulijutia.
Kama kiongozi ambaye anapaswa kutoa dira ya uongozi wa chama, Mtatiro, pamoja na mambo mengine, alipaswa kufahamu kuwa ni nani adui wa chama na ana nguvu kiasi gani. Wakati ule Mtatiro alimhesabu Profesa Lipumba kama mmoja wa maadui wa chama hicho lakini akafanya kosa kubwa sana la kumdharau adui huyo.
Kauli alizokuwa anazitoa wakati huo zilionesha kana kwamba Profesa Lipumba na kundi lake wasingeweza kufanya chochote cha kukiathiri chama hicho, lakini leo tunashuhudia mambo yanayofanywa na Profesa Lipumba ambayo yameiweka CUF katika nafasi ngumu sana.
Lipumba ambaye Mtatiro aliwataka wanachama wa CUF wampuuze, kwanza alifanikiwa kusimamisha akaunti ya chama na kufungua akaunti mpya ambayo inatumika kupitisha ruzuku ya chama hicho(swala hili bila shaka lilifanya uongozi wote uliokuwepo bila yeye – kuanzia kwa Makamu Mwenyekiti kushuka chini kupata ukata wa hali ya juu hivyo kukosa kabisa nguvu ya kupambana naye), Pili akafanikiwa kukamata ofisi za Makao Makuu ya chama yaliyopo Buguruni, jijini Dar es salaam na tatu akafanikiwa kufuta bodi ya wadhamini ya CUF na kupitisha bodi mpya.
Kama hilo halitoshi, Profesa Lipumba ambaye Mtatiro alitaka apuuzwe, ndiye anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kama kiongozi mkuu wa CUF.
Juzijuzi hapa, Lipumba alifanikiwa kuwafukuza wanachama nane wa chama hicho ambao pia walikuwa ni wabunge wa viti maalum na kwa kufukuzwa huku, wamepoteza nafasi yao ya ubunge na amefanikiwa kuteua watu ambao wanaonesha kumuunga mkono kujaza nafasi hizo bungeni.
Pamoja na hayo, ni Lipumba huyu huyu aliyeamua kumuweka kando kwa muda Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad na nafasi yake kushikwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya – jambo ambalo linaweza kudhihirika wazi kuwa ni mahesabu mazito ya kudhoofisha kambi ya Maalim Seif na Mtatiro kwakuwa ndiyo iliyojiunga kumpiga vita Lipumba kwa muda wote huu.
Kwa hakika, kabla Mtatiro hajawaambia wanachama wampuuze Lipumba, alipaswa kufahamu nguvu aliyonayo au iliyopo nyuma ya Profesa Lipumba. Ufahamu huo ungemuwezesha Mtatiro kama kiongozi mkubwa kwenye chama kufahamu anapambana na nani.
Lakini inavyoelekea Mtatiro hakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu nguvu ambayo Profesa Lipumba alikuwa nayo. Inaonekana yeye akatimiza kwa vitendo kile ambacho aliwataka wanachama wengine wa CUF wakifanye – kumpuuza Profesa Lipumba. Matokeo yake, yule aliyeamua kumpuuza leo hii amekuwa tishio kubwa kwa uhai wa chama hicho.
Kama Mtatiro angekuwa makini tangu mwanzo, kamwe hakupaswa kumpuuza Profesa Lipumba. Alitakiwa kuwa na mikakati ya kuhakikisha kuwa Profesa Lipumba na kundi lake hawaleti madhara katika chama. Lakini kwa bahati mbaya sana inaonekana Mtatiro hajalifahamu kosa lake kwa sababu mpaka leo bado anaendelea na kauli yake hii ya kuwataka wana CUF wampuuze Profesa Lipumba.
Kwa bahati mbaya sana Mtatiro na wenzake wamechelewa sana kurekebisha kosa lao. Hivi sasa Profesa Lipumba na kundi lake tayari wameshaanza kuweka mizizi na ni kazi kubwa sana kuwaondoa bila kukiharibu chama hicho.
Awali ilionekana kuwa Profesa Lipumba na wenzake ndio walikuwa wakipigania uhai wao, lakini sasa hali imegeuka na ni Mtatiro na wenzake ndio wanaonekana wanapigania uhai wao ndani ya CUF. Kama Profesa Lipumba asingepuuzwa, haya yasingetokea.
HT @ MTANZANIA