Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa kuna mkakati unaosukwa kuihusisha waganga wa kienyeji kutoka Naijeria, Sumbawanga, Pemba na Unguja kwa lengo la kutaka kumuua.
Maalim Seif alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho Wilaya ya Magharibi A, Unguja.
“Juzi nasikia wamejaza meli ya Mapinduzi II. Kulikuwa na mkutano wa wananchi waliokuwa nje ya nchi, nadhani ni Dayaspora. Kulikuwa na mkutano uliofunguliwa na January Makamba kwa niaba ya Makamu wa Rais.
Jioni yake wakatiwa kwenye meli eti wanatembezwa kwenye visiwa mpaka mkondo wa Nungwi, meli ikasimama kwa saa mbili, ndani kuna kamati ya ufundi iliyoundwa na watu kutoka Naijeria, Sumbawanga, Pemba na Unguja, kumbe wanafanya kazi zao huku wanasema Dayaspora,” alisema Seif.
“Waganga hao wamepewa kazi nyingine, kuhakikisha wanamwondoa Maalim Seif duniani na nimeambiwa na wahusika wenyewe. Kwahiyo wenzetu kwa sasa wako hamkani hasa wakizingatia nilitoa miezi mitatu, sijui imebaki siku ngapi sasa.”
Aliwaambia wajumbe hao kuwa katika kipindi hiki watashuhudia mambo mengi ya kuzuia haki yao isipatikane lakini nguzo yao ni Mwenyezi Mungu kwakuwa hawana njia nyingine.
“Ukisimama kwenye nguzo ya Mwenyezi Mungu huwezi kuanguka. Wengine mna wasiwasi Mahakama iko upande wa Lipumba. Ninawaambia Mahakama haipo upande wowote, inatenda haki.
“Chama chetu sasa hivi kinapita katika kipindi kigumu. Kuna hujuma za Lipumba na genge lake ambao wote tunajua nyuma yake ni dola na ninyi ni mashahidi jinsi gani dola inavyomuunga mkono,” alisema Seif.