SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 15 Agosti 2017

T media news

Lipumba Bado Amng'ang'ania Maalim Seif Kujisalimisha Ofisini Kwake

Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba ameendelea kumtupia lawama katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kwa madai kuwa amejenga chuki dhidi yake.

Amesema mara kwa mara amekuwa akimpigia simu katibu huyo kwenda ofisini kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake, lakini hapokei na mara mwisho alimpigia Machi mwaka huu.

Profesa Lipumba ameeleza hayo leo Jumanne Agosti 15 wakati akizungumza na wanahabari kuhusu mwenendo wa chama hicho na kuyatolea ufafanuzi masuala mbalimbali yanayoendelea ndani ya chama hicho.

Amesema Maalim Seif amekuwa na chuki dhidi yake hadi kufikia hatua ya kufungua kesi kwa hati ya dharura dhidi ya uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi la upande wa Profesa Lipumba.

Hivi karibuni baraza hili liliwavua uanachama wabunge wa viti maalumu wanane na madiwani wawili viti maalumu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

"Hakuwa sahihi kwenda kufungua kesi mahakamani, wakati haya mambo tungeweza kukaa na kujadiliana hizi ndiyo chuki ninazozisema. Lakini namwambia suluhu haiwezi kuisha kwa kila mtu kuwa kivyake badala ya yeye kuja ofisini kutekeleza majukumu," amesema Profesa Lipumba.

Kuhusu majina ya wabunge wanane walioteuliwa hivi karibuni Profesa lipumba amesema uteuzi huo ulifuata taratibu zote kwa mujibu wa Katiba ya CUF na kwamba majina hayo yalikuwepo katika orodha iliyopelekwa na Maalim Seif mwaka 2015.

Hata hivyo, Profesa Lipumba amesema chama hicho ndiyo mkombozi pekee wa vyama vya upinzani kwa kuwa kina hoja za kuwasimamia Watanzania kwani wengine wameshindwa.