Taarifa ambazo zimethibitishwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, orodha hiyo ya viwanda vilivyotelekezwa itawekwa hadharabni mjini Dodoma kesho na wahusika kunyang’anywa viwanda hivyo kabla hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa.
Aidha, Nipashe imebaini kuwa wale watakaobainika kuwa walifanya udanganyifu kwa kutumia viwanda walivyopewa kutwaa mikopo ya mabilioni ya fedha na kwenda kuzitumia kwa mambo mengine, sasa wako kitanzini kwa sababu mchakato wa kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria utaanza mara moja, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli.
Hivi karibuni, magereza ya Keko na Segerea yamejitwalia umaarufu kwa kuwapokea mahabusu mbalimbali wanaotuhumiwa kwa kesi zinazohusiana na uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, ambazo huwa hazina dhamana.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha saruji cha Kilimanjaro wilayani Korogwe, Jumapili, Rais Magufuli alimtaka Waziri Mwijage awanyang’anye viwanda wale wote waliovitelekeza bila kuviendeleza kwa miaka 20 na pia kutaka ufanyike utaratibu wa kuwatoza faini na kuwapeleka jela wale watakaoshindwa kueleza ni wapi walikopeleka mabilioni ya fedha waliyokopa benki kwa kutumia viwanda hivyo.
“Tuliwapa viwanda marafiki zetu kwa kuangalia sura… sasa wewe Waziri usiangalie sura ya marafiki wa wenzako waliotangulia, we wakung’ute sawa sawa. Hicho ndicho ninataka mkafanye wewe na makatibu wako, atakayeenda mahakamani tutajua namna ya ku-‘deal’ naye, sheria zipo.
Tutamwingizia kesi ya uhujumu uchumi,” alisema Rais Magufuli.
Kupitia chanzo chake, Nipashe ilielezwa kuwa miongoni mwa watuhumiwa wa ‘upigaji’ wa mabilioni hayo ya fedha za viwanda kutoka kwenye taasisi mbalimbali za fedha, wamo baadhi ya vigogo wenye majina makubwa katika maeneo mbalimbali.
“Kama alivyosema Rais (Magufuli) wakati akiwa Tanga. Yeyote aliyetwaa kiwanda na kukitumia kukopa fedha benki kwa matumizi yake mengine, sasa atakuwa shakani… ni kwa sababu atafikishwa kwenye mkono wa sheria bila kujali yeye ni nani,” chanzo kiliiambia Nipashe jana, kikirejea maelekezo ya Rais kwa Waziri Mwijage.
Hata hivyo, Nipashe haikufanikiwa kupata chanzo huru kuthibitisha juu ya madai ya kuanza kwa mchakato wa kuwafikisha kortini na hatimaye mahabusu wale wote watakaokumbwa na tuhuma za kutwaa fedha benki kwa kutumia jina la viwanda ilhali wakivitelekeza na kuzitumia kwa masuala yao mengine.
WAZIRI MWIJAGE AFUNGUKA
Alipoulizwa na Nipashe kuhusiana na utekelezaji wa amri ya Rais juu ya viwanda vilivyotelekezwa, Waziri Mwijage alisema wale walioshangilia yeye kubanwa na Rais Magufuli mbele ya hadhara mkoani Tanga, wataumbuka Alhamisi (kesho) wakati atakapotaja viwanda ambavyo ameshavirejesha serikalini.
Mwijage alisema kuwa kesho, atazungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma na kuweka hadharani orodha ya viwanda ambavyo amevirejesha serikalini, vikiwamo vilivyobinafsishwa miaka mingi iliyopita na wawekezaji walioviendeleza.
Akifafanua zaidi jambo hilo, Mwijage alisema kazi waliyoifanya kuhusiana na agizo la Rais ni kubwa na kwamba kesho ndiyo atawaweka hadharani wahusika.
“Unajua bondia mzuri ni yule ambaye anakubali kupigwa angalau kidogo ili baadaye akiinuka na kuanza mashambulizi watu washangae. Sasa watu walifurahia mimi kusemwa. Lakini sasa wataona mambo,” alisema Mwijage.
Aliongeza kuwa amri ya Rais huwa haijadiliwi na kwa wale waliolelewa kwenye maadili kama yeye, wakiagizwa na mtu mkubwa kama Rais kinachofuatia ni utekelezaji, kama ambavyo amefanya kwenye eneo la kuchukua viwanda ambavyo havijaendelezwa kwa miaka mingi.
“Kama una mwandishi wako mlete Alhamisi Dodoma uone mambo… maana nitatoa picha nzima ilivyo,” alisema Mwijage.
Mwijage alisema tangu Rais Magufuli atoe agizo la kuchukua viwanda ambavyo havijaendelezwa, yeye na wataalamu wake wamekuwa hawalali kuhakikisha azma hiyo inatimia mapema iwezekanavyo.
“Kazi kubwa inafanyika chini kwa chini na kwa taarifa yako, wenye viwanda wengine wamekuwa wakiagiza mashine za kufufua viwanda hivyo kwa ndege na wamekuwa wakifanya kazi hiyo usiku na mchana na vingine vimeshaanza kufanya kazi,” alisema Mwijage.
JPM ALIVYOMBANA MWIJAGE
Akizungumzia suala hilo mjini Tanga, Rais Magufuli alielezea kushangazwa kwake na viongozi wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kutowajibika katika kuwachukulia hatua wamiliki waliotelekeza viwanda.
“Uko wewe waziri, makatibu wakuu wawili, mwingine ni profesa mwingine ni dokta… yupo Naibu Katibu Mkuu ambaye ni Injinia. Sijasikia viwanda vikifutwa,” alisema Rais na kuongeza:
“Kwenye hilo unanikwaza. Nataka nisikie watu wananyang’anywa viwanda na usiogope, mmiliki wa kiwanda awe wa CCM, CUF, au
Waziri, yeyote we nyang’anya. “Sitaki haya mambo niwe narudia rudia, sipendi… nimekueleza tukiwa wachache ofisini nikajua utanisikia, lakini bado.
“Nimezungumza kwenye Baraza la Mawaziri bado, nimezungumza hadharani bado. Sasa unataka nizungumzie nikiwa kaburini?
“Waziri ninakuomba, nimezungumza mara nyingi… sitaki kuzungumza zaidi.”