Jukwaa la Wahariri (TEF) leo limetangaza kuondoa zuio la kutangaza habari za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda huku yeye akikataa kuomba radhi na kusema kuwa yaliyopita yamepita na sasa tugange yajayo.
Hayo yameibuka leo katika mkutano wa pamoja wa Makonda na TEF, ambao hapo awali walitangaza uamuzi wa kutoshirikiana na Mkuu huyo wa Mkoa kwa kutotangaza habari zinazomhusu kufuatia madai ya kuvamia kituo cha luninga cha Clouds Media Group na kumtaka aombe radhi.
Kwa mujibu wa Katibu wa TEF, Theophil Makungu, Makonda amekiri kuwa tukio hilo lilitokea lakini dhana ya wakati tukio lilipotokea haikuwa kama ilivyochukuliwa lakini akamtaka kuomba radhi.
Hatahivyo Mkuu huyo wa Mkoa alikataa kuomba radhi kama ambavyo TEF ilikuwa inataka tangu awali.
“Ndugu waandishi wa Habari na Wahariri, kile ambacho Katibu amekisema hakitatokea kwenye kinywa changu, sitaomba radhi,” amesema Makonda.
TEF imesema kuwa walichokisikia mara ya kwanza kilitoka Clouds lakini hawakupata nafasi ya kusikiliza kutoka kwa Mkuu wao wa Mkoa na hivyo mahusiano kati ya waandishi wa habari na yeye (Mkuu wa Mkoa) yaende vizuri kuanzia sasa na kuendelea.
Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba amesema kuwa TEF haiwezi kusema kuwa ilipokuwa inazungumza na Mkuu wa Mkoa, haikupata upande wa pili, upande wa pili ulikuwepo na jambo hili liliripotiwa.
“Hatuko sawa kwasababu kwanza TEF haijawahi kutafuta nafasi ya kusikiliza upande wangu,” amesema Ruge.
Haya yanajiri siku chache baada ya Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kuwaita jukwaani Makonda na Ruge na kuwataka kumaliza tofauti zao kwa kushikana mikono.