Rais wa Afrika Kusini amenusurika kwa mara nyingine katika kura ya kutokuwa na imani naye iliyopigwa na bunge la nchi hiyo ambapo awamu hii ilikuwa ni ya tofauti kwani ilikuwa ni kura ya siri.
Rais Zuma kwa vipindi mfululizo ameshuhudia maandamano na kura za kutokuwa na imani zikipigwa kwa lengo la kumtaka ajiuzulu kutokana na tuhuma mbalimbali za rushwa na upendeleo zinazomkabili.
Kutokana na kura zilizopigwa jana na bunge la nchi hiyo, jumla ya kura hizo ni 384 huku waliosema hawana imani naye wakiwa 177, wenye imani wakiwa ni 198 na kura zilizoharibika ni 9.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, Wabunge 40 wa chama tawala, ANC wamepiga kura ya kutokuwa na imani na Rais Jacob Zuma hivyo kutaka ang’atuke.
Viongozi mbalimbali wa ANC pamoja na wabunge wengine wa chama hicho, wametaka wabunge hao (40) wachukuliwe hatua za kinidhamu kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kukisaliti chama.
Muda mfupi baada ya bunge kutangaza matokeo hayo yaliyokuwa yakisubiriwa kwa hamu, wafuasi wa Rais Zuma walionekana wakicheza na kuimba kwa furaha nje ya jengo la bunge wakisherehea ushindi huo.
Aidha, kwa upande mwingine imeripotiwa kuwa, fedha ya Afrika Kusini (Rand) imeporomoka kwa zaidi ya asilimia 1 baada ya kutangazwa kuwa Rais Zuma ameshinda kwenye kura hiyo.
ANC imempongeza Rais Zuma kufuatia ushindi huo huku kikisema kwamba, mara zote kimekuwa kikitoa makada wenye kuaminika katika nafasi za serikali.
Rais Zuma amepigiwa kura ya kutokuwa na imani naye kwa zaidi ya mara 5 ambapo mara zote amefanikiwa kuruka kiunzi na kuendelea kusalia madarakani.