Shirika la Umeme nchini (TANESCO) limedaiwa kugomea zoezi la ukataji umeme kwenye nyumba zinazotakiwa kuvunjwa eneo la Kimara na Kiluvya ili kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro leo Jumatatu, Julai 31 kwa kile kinachoelezwa na shirika hilo kuwa Tanroads hawajajipanga.
Mratibu wa bomoa bomoa, Ephrahim Kinyafu amesema Tanroads wameweka kambi eneo hilo tangu saa nne asubuhi wakiwasubiri Tanesco kuendelea na zoezi la kukata umeme lakini hawajafika, walipompigia simu Meneja wa Tanesco Kimara, Christopher Nguma akadai hawawezi kuwakatia umeme wateja wao.
“Tanesco pia wamegoma baada ya kutoa taarifa yetu jana kwamba suala letu la bomoabomoa liko mahakamani kwahiyo wanasema kama tunakesi mahakamani basi hawatakata umeme, “,amesema Kinyafu kwenye Mahojiano yake na Gazeti la Mwananchi.
Hata hivyo, Kinyafu amesema sababu nyingine waliyoieleza Tanesco ni kuwa utaratibu wa kuwakatia umeme unaambatana na kutoa notsi ya saa 48, lakini hawajatoa na badala yake Tanroads wanawataka wakakate umeme kitu ambacho hakiwezekani.