Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni jana tarehe 05 Agosti, 2017 wameweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Sherehe za uwekaji jiwe la msingi la mradi huo zilifanyika katika Kijiji cha Chongoleani Wilayani Tanga na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu wa Pili wa Waziri Mkuu wa Uganda Mhe. Dkt. Ali Kirunda Kivejinja, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wabunge na viongozi wa taasisi za Serikali za Tanzania na Uganda pamoja na wakuu wa mikoa ya Tanzania.
Bomba la kusafirisha mafuta hayo lenye urefu wa kilometa 1,445 ambapo kilometa 1,115 kati yake zitajengwa Tanzania, litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 kwa siku na ujenzi wake umepangwa kukamilika mwaka 2020 kwa gharama ya takribani Shilingi Trilioni 8 za Kitanzania.
Bomba hili litajengwa na kuendeshwa na kampuni za TOTAL ya Ufaransa, CNOOC ya China na TULLOW ya Uingereza, kwa ubia na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi Mhe. Rais Magufuli alimshukuru Mhe. Rais Museveni na Serikali yake kwa kufanikisha mradi huo na amemhakikishia kuwa Tanzania imejipanga kutoa ushirikiano wa kutosha pamoja na kuilinda miundombinu ya mradi huo.
Mhe. Rais Magufuli aliwataka wananchi watakaonufaika na ajira zaidi ya 30,000 zitakazozalishwa na mradi huo kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na uaminifu na pia ametoa wito kwa wananchi wa Tanga na mikoa yote itakayopitiwa na mradi huo kujipanga kunufaika na fursa mbalimbali za biashara zitakazotokana na mradi huo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekubali ombi la Mhe. Rais Museveni la Tanzania kujenga bomba la kusafirisha gesi kwenda nchini Uganda kwa ajili ya kusaidia uzalishaji wa chuma, na pia amemshukuru kwa kukubali kutoa wataalamu waliogundua mafuta nchini Uganda kuja kushirikiana na wataalamu wa Tanzania kwa ajili ya kufanya utafiti wa mafuta katika ziwa Tanganyika na ziwa Eyasi magharibi mwa Tanzania.
"Kutoka Msimbati Mtwara mpaka Uganda kuna kilomita 1422, kwa hiyo kuweka bomba ambalo litapitisha gesi wakati hili lingine linapitisha mafuta, inashindikana nini? Napenda kumuhakikishia muheshimiwa haya yanawezakana, bomba la gesi lipite hapa kwenda Uganda, Kama wao wametukubalia kwa nini sisi tushindwe, huu ndio ushirikiano wa Afrika Mashariki , Tuwapelekee gesi wakafufue viwanda vyao vya chuma kule", alisema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mhe. Rais Museveni amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa utayari wake wa kutekeleza mradi huo, na amesisitiza kuwa Tanzania na Uganda zinapaswa kushirikiana katika fursa zake mbalimbali ili kujenga uchumi imara na kuboresha maisha ya watu wake.
Mhe. Rais Museveni alitolea mfano wa mradi wa bomba la mafuta ghafi litakalojengwa na kueleza kuwa mafuta yatakayozalishwa yataziwezesha nchi hizi na nyingine za Afrika Mashariki kupata mafuta kwa gharama nafuu na hivyo kuimarisha huduma za usafirishaji na viwanda, na pia alisisitiza kuwa Tanzania iliyogundua gesi nyingi itaiuzia Uganda ili iitumie kuzalisha chuma kingi na kukiuza Tanzania.
Mhe. Rais Museveni pia alitoa wito kwa nchi za Afrika Mashariki kushirikiana zaidi na kujipanga kukabiliana na changamoto ya uwiano wa kibiashara usio na manufaa kwake, kutokana na takwimu kuonesha kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki inauza kiasi kidogo cha bidhaa ikilinganishwa na bidhaa zinazoingia kutoka nje.
Mhe. Rais Museveni amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku 2 hapa nchini na amerejea nchini Uganda, na Mhe. Rais Magufuli leo anaendelea na ziara yake ya siku 5 hapa Mkoani Tanga ambapo atazindua kiwanda cha saruji cha Kilimanjaro, ataweka jiwe la msingi la upanuzi wa kiwanda cha maziwa cha Tanga (Tanga Fresh) na ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa matanki ya kuhifadhia mafuta katika eneo la Raskazone hapa Mjini Tanga