Mkazi wa Mtaa wa Makanyagio katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, Beatrice Kangu (48) amekufa muda mfupi baada ya kutoa sadaka katika ibada ya Jumapili iliyofanyika katika Kigango cha Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda kilichopo katika Mtaa wa Makanyagio B.
Akizungumzia mkasa huo, Mwenyekiti wa kigango hicho, Charles Kanyanda alisema Kangu ambaye ni mwanakwaya, alikuwa muumini wa Kanisa Katoliki, na Jumapili alihudhuria ibada ya Misa Takatifu kwenye kigango hicho ambayo ilifanyika saa moja na nusu asubuhi.
Alisema Beatrice alihudhuria ibada ya misa hiyo ambapo kwa kuwa alikuwa mwanakwaya aliingia kwenye nyumba ya ibada na kujiunga na wanakwaya wenzake iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu wa Dini (Katekista) wa Kigango, Agustino Ntalwila.
“Ibada ya Misa Takatifu iliendelea kama kawaida na ndipo ilipofikia muda wa kutoa sadaka na Beatrice alikwenda kutoa sadaka kama kawaida kisha akarudi kwenye nafasi yake na kuendelea kuimba ghafla baadaye alianguka na kupoteza fahamu.
Taharuki iliibuka kwenye nyumba hiyo ya ibada ndipo ilipobainika kuwa alikuwa amekata roho,” alieleza Kanyanda na kuongeza kuwa wanakwaya wenzake walijitahidi kumpatia huduma ya kwanza bila ya mafanikio.
Kanyanda alisema maziko yake yalifanyika katika makaburi ya Mwanga jana ambayo yaliongozwa na Paroko wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Maria Imakulata, Monsinyori, Padri George Kisapa aliyemwelezea alikuwa mcha Mungu na ameacha pigo kubwa kwenye kwaya ya Kigango cha Makanyagio B.