Mimi VUTA-NKUVUTE alias Mzee Tupatupa, kada nguli wa CCM na 'Shushushu' mstaafu, nampongeza Rais na Mwenyekiti wangu wa CCM Dr. John Pombe Magufuli kwa anachokifanya sasa kuhusu madini. Nampongeza Rais kwa kuanzisha 'vita' hii ya kusaka haki yetu kama Taifa na kupata tunachostahili.
Mhe. Rais, nimekusikiliza vya kutosha bila kutisha. Nakupongeza hasa kwa kuliona tatizo linalozunguka mambo yote haya: ubovu wa Sheria zetu mbalimbali zinazosimamia madini. Hakuna haja ya kunyoosheana vidole kwa wale waliokuwa wakijadili tofautitofauti lakini kwa hoja moja ya ubovu wa sharia.
Mhe. Rais, kuhusu wahusika waliotajwa na Kamati Maalum ya Prof. Osoro leo, ulipaswa kuagiza kwa kutaja majina wahusika wa kuhojiwa. Wametajwa wengi kwenye Ripoti, kwa mazuri na mabaya. Wametajwa wasiotajika na watahojiwa wasiohojika. Madini ni yetu sote. Tutayalinda hadi tone la mwisho la damu yetu kama watanzania. Tulitaka Rais uanze.
Mhe. Rais, umefanya vyema kumkabidhi kazi ya kisheria Nguli wa Sheria, Prof. Kabudi. Yeye anawajua waliokuwa wanafunzi wake bora, imara, waaminifu na walinda maslahi ya nchi. Anawajua waliopo Serikalini na wale walio sekta binafsi. Anawajua waliopo chamani-CCM na wale waliopo upinzani. Kwakuwa hili sasa ni jambo la kitaifa, atawachagua kutoka popote.
Kuwa na 'neutral pool' ya Wanasheria wazalendo ni jambo kubwa na la kupongezwa. Ulinzi wa nchi kiuchumi upo kwenye sheria. Mhe. Rais, ulipaswa kuwataja wakuhojiwa waziwazi: Chenge, Yona, Salula, Mwanyika, Kafumu na kadhalika. Kwakuwa wote ni wanaCCM, nakushauri uwashughulikie pia kichama ili 'kukisafisha' chama.
Tutalinda mali zetu, tulisubiri Rais alianzishe!
Mzee Tupatupa wa Lumumba, Dar es Salaam