SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 12 Juni 2017

T media news

Makala: Wasomi Watanzania walioletwa na JK kutoka nje na kutumbuliwa na JPM

Kufukuzwa kwa Profesa Muhongo Mei 24 kumeleta mjadala mkubwa kutaka kujua ni kwa nini wataalamu wetu walioletwa kutoka nje kutumikia nchi yao hawadumu Serikalini.

Mei 24, 2017, Rais Dkt. John Magufuli alibatilisha uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo muda mfupi baada ya kukabidhiwa ripoti ya makinikia ya mchanga wa madini na Mwenyekiti wa Kamati ya wataalamu, Profesa Abdulkarim Mruma.

Ripoti hiyo iliyoonesha kuwa kuna tofauti kati ya kiwango cha madini kilichoorodheshwa kwenye nyaraka na kile kilichokutwa kwenye mchanga wenyewe ambacho kinakadiriwa kuwa na thamani kati ya shilingi bilioni 829.4 na trilioni 1.439 kutokana na mchanga uliokuwa kwenye makontena 277 yaliyokuwa yasafirishwe kwenda nje ya nchi.

Kutumbuliwa kwa Profesa Muhongo, msomi nguli wa taaluma ya miamba aliyefundisha katika vyuo vikuu vyenye hadhi kubwa sana duniani kumeibua mjadala kujua kwa nini wasomi wetu wa hali ya juu kiasi hiki wenye heshima za kipekee duniani ambao wamerudi/kurudishwa kuitumikia nchi yao hawadumu sana kwenye serikali.

Mbali na Profesa Muhongo, viongozi wengine wa juu ambao pia ni wataalamu waliorudi kuitumikia nchi na hawakudumu ni pamoja na Rished Bade (aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania – TRA), Juliet Kairuki (aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Uwekezaji ya Taifa – TIC) na Dkt. James Mataragio (aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini – TPDC).

Wataalamu hawa walirudishwa na serikali ya awamu ya nne iliyoongozwa na Rais Dkt. Jakaya Kikwete. Kwa mujibu wa taarifa rasmi, Rais Kikwete alishangazwa alipokuta Watanzania hawa wakiwa kwenye nafasi za juu za uongozi kwenye taasisi na mashirika ya kimataifa alipokuwa kwenye safari zake za nje ya nchi na kuamua kuwaomba baadhi yao warudi kuongeza ufanisi Serikalini.

Profesa Makame Mbarawa ni mtaalamu mwengine aliyeombwa kurudi na Dkt. Kikwete na mpaka sasa yupo Serikalini kama Waziri wa Miundombinu na Usafirishaji. Wasomi kutoka vyuo mbalimbali nchini pia wamekutana na hatma kama hii ambayo inawakuta wenzao waliotoka nje ya nchi kwakuwa wao pia hawajadumu sana kwenye nafasi zao pamoja na kuacha nafasi zao za heshima kwenye taasisi za elimu walipotoka.

Profesa Muhongo

Rais Kikwete alimteua Profesa Muhongo mwaka 2012 kuwa Mbunge kisha kumteua kuwa Waziri wa Nishati na Madini akichukua nafasi ya William Ngeleja aliyejiuzulu. Kabla ya uteuzi huu, Muhongo alifanya kazi katika taasisi kadhaa ndani na nje ya nchi zinazohusu masuala ya miamba ikiwemo Taasisi ya Miamba Afrika ambapo alikuwa ni Rais wa Taasisi hiyo kuanzia mwaka 1995 hadi 2001, Mwenyekiti wa Bodi ya Unescco kuhusu Programu ya Kimataifa kuhusu Sayansi ya Miamba (2004-2008) na Mwenyekiti wa Programu ya kamati ya Siasa ya Mwaka wa Kimataifa wa Sayari ya Dunia (2007-2010.

Lakini kutumbuliwa kwake hiyo Mei 24 haikuwa mara ya kwanza kwake. Alilazimika kujiuzulu mwezi Januari mwaka 2015 alipoamua kuwajibika kutokana na skendo ya Escrow ambapo zaidi ya Dola za Marekani milioni 100 zilikombwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambapo Naibu wake, George Simbachawene.

Alirudishwa kwenye nafasi yake hiyo mwezi Disemba mwaka 2015 baada ya kuteuliwa na Rais wa sasa, Dkt. John Magufuli.

Dkt. James Mataragio

Dkt. Mataragio aliteuliwa na Rais Kikwete Disemba 2014 kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli (TPDC). Kabla ya uteuzi huu, alifanya kazi kama mwanasayansi wa masuala ya miamba katika Taasisi ya Bell Geospace ya nchini Marekani kwa miaka 10. Akiwa anafanya kazi Bell Geospace, Dkt. Mataragio alijitolea kuwa mshauri wa serikali kuhusu madini na gesi asilia.

Alisimamishwa mwaka 2016 baada ya ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kubaini matumizi mabaya katika Shirika hilo.

Rished Bade

Alijiunga TRA kama Kamishna Mkuu Msaidizi wa Mamlaka hiyo mwezi Septemba mwaka 2012 mpaka mwaka 2014 alipopandishwa cheo na kuwa Kamishna Mkuu, akichukua nafasi ya Harry Kitilya aliyestaafu mwaka 2013.

Kazi yake kama bosi mkuu wa TRA iliisha Novemba mwaka 2015 muda mfupi baada ya ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika Bandari ya Dar es salaam ambapo alibaini upotevu mkubwa wa mapato ya serikali yaliyofanywa na maafisa wa bandari kavu wakishirikiana na maafisa wenzao wa Mamlaka ya Bandari (TPA) na TRA ambapo iligundulika kuwa makontena yalisharuhusiwa kutoka bandarini hapo hayakuwa yamelipiwa ushuru stahiki.

Bade ana Shahada ya Biashara na Uongozi kutoka Chuo Kikuu Dar es salaam (1995), Shahada ya Uzamili kuhusu masuala ya Uendeshaji wa Mabenki na Fedha kutoka Chuo Kikuu cha Sydney (1999), pia ana leseni ya Ukaguzi wa Mahesabu.

Alianza kazi mwaka 1995 katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kama Mkaguzi wa mabenki ambapo alifanya kazi kwa miaka mitano kisha akajiunga na Akiba Commercial Bank (ACB) mwezi Juni mwaka 2000 kama afisa mikopo. Mwaka mmoja baadae alijiunga na Benki ya Barclays Tanzania kama Mkurugenzi wa Fedha, nafasi aliyoishikilia kwa miaka mitano kabla ya kwenda Barclays Uganda mwaka 2007.

Mwezi Disemba mwaka 2009 aliteuliwa kuwa Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki za Barclays kwa nchi za Mashariki na Magharibi mwa Afrika, Makao Makuu yakiwa jijini Nairobi, Kenya.

Juliet Kairuki

Alitumbuliwa mwaka jana kwa kosa la kutochukua mshahara toka mwezi Aprili mwaka 2013 alipoteuliwa. Katika taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda akiwa anatangaza kutumbuliwa kwa Kairuki alisema:

“Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Juliet Kairuki kama Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Uwekezaji Tanzania kutokana na sababu nyingi ikiwemo baada ya Rais kupewa taarifa kuwa hakuchukua mshahara wa serikali tangu uteuzi wake tarehe 24 Aprili mwaka 2013 mpaka sasa, jambo linaloibua maswali mengi.”

Kabla ya hapo, alikuwa akifanya kazi nchini Afrika Kusini kwa miaka 12, kumi kati ya hiyo ni katika sekta ya benki akiwa kama Meneja Mkuu wa Chama cha Mabenki nchini Afrika Kusini akiwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa miradi muhimu kwenye ukanda wa SADC.

Kairuki ni mtaalamu aliyebobea kwenye miundombinu ya kifedha kwenye miradi ya ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi na ana historia ya taaluma ya Sheria na alishawahi kufanya kazi kama wakili wa Serikali. Alipata Shahada yake ya Sheria nchini Tanzania na Shahada ya Uzamili (Masters) ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Cape Town nchini Afrika Kusini.

Akizungumzia kutumbuliwa kwa wataalamu hawa, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Dkt. Aidan Msafiri alisema kuwa wataalamu hawa walitumbuliwa kutokana na makosa ya kimaadili au uwezo mdogo, na hili halijalishi kama mtu ameshawahi kufanya kazi kwenye taasisi maarufu za kimataifa.

“Unaweza kuwa na vyeti vizuri sana lakini haitoshi kumfanya kuwa muadilifu na mzalendo,” alisema Dkt. Msafiri.