SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 12 Juni 2017

T media news

CHADEMA Wampa Kazi Mke wa Lowassa

Wanawake wa Chadema wamemtwishwa Regina Lowassa mzigo wa kuongoza mapambano ya ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Akizungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Wanawake wa Chadema (Bawacha) mjini Dodoma jana, Regina ambaye ni mke wa waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa, alisema maandalizi ya uchaguzi huo yanapaswa kuanza sasa.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Lowassa aligombea urais kupitia Chadema kwa kushirikiana na vyama vilivyounda umoja wa katiba ya Wananchi (Ukawa) na hivyo kuweka ushindani mkubwa dhidi ya chama tawala, ingawa hakushinda.

Jana, Regina alisema ushindi wa chama hicho uko mikononi mwa wanawake wa Tanzania. “Kwanza niwashukuru sana kwa mapambamo mliyoyafanya mwaka 2015. Nataka mfahamu kuwa bado Chadema inapendwa na ina nguvu kubwa kuliko wakati mwingine. Msikatishwe tamaa bali tusonge mbele,” alisema Regina.

Mama huyo aliwataka wajumbe kujiamini zaidi na kupeleka ujumbe kwa wenzao ambao wamedhamiria kufanya mageuzi makubwa, lakini akawataka wasilale.

Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee aliwataka wanawake kujitoa zaidi katika kukisaidia chama hicho, hasa katika maandalizi ya uchaguzi ujao.

Mdee aliwashauri wanawake wenye nafasi, kama wabunge, kutumia nafasi zao kukisaidia chama.

Alisema wakati walionao kwa sasa si wa kujivunia nafasi walizonazo, bali wanapaswa kuongeza nguvu zaidi na kugombea nafasi za uongozi wa juu wa Chadema ili waendeleze mapambano ya ukombozi.

“Katika kipindi hiki ambacho tunaona demokrasia inaminywa kwa vyama vyote vya siasa, ni vema wanawake ambao ni jeshi kubwa tukawa mstari wa mbele katika mapambano si kurudi nyuma. Lazima kuwa na nidhamu ndani na nje ya chama ili tufanikiwe katika vita hii,” alisema Mdee.

Katika kuonyesha msisitizo huo, alimuagiza katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega kuwaandikia barua wabunge ambao hawakuhudhuria kikao cha jana ili wajieleze kabla ya kuchukuliwa hatua.

Alisema ni jambo la aibu na fedheha kwa viongozi kutoka mbali wakasafiri hadi Dodoma kwa ajili ya kikao, lakini wabunge ambao wako mjini hapa wakashindwa kuhudhuria.

Mbunge wa Viti Maalumu, Devotha Minja alisema chachu ya ushindi na mapambano ndani ya chama hicho kwa sasa ni kubwa kwa kuwa wameamua kufanya kazi usiku na mchana kwa ajili ya kuisaidia Chadema.