JUMA KASEJA-KAGERA SUGAR.
ZIKIWA zimesalia mechi chache kabla ya kuhitimisha msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2016/17, wapo magolikipa waliofanya vizuri mpaka sasa.
Ingawa msimu huu haukuwa na kiwango kikubwa cha makipa wapya kuibuka na kuteka hisia za mashabiki au baadhi ya viongozi wa timu kubwa kuanza kuwamezea mate, wale wa zamani wameonekana kuokoa jahazi.
Makipa wengi wa Ligi Kuu msimu huu wameonekana kuwa ni wa kawaida sana, wakiwa na makosa mengi, wakifungwa mabao rahisi, pia wakishindwa hata kupanga mabeki wao sawasawa, wakati wanashambuliwa au kupigiwa mipira ya faulo.
Wafuatao ni makipa ambao wao angalau wameitoa kimasomaso Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuonekana kufanya vema langoni.
1. Juma Kaseja-Kagera Sugar
Kwa zaidi ya miaka 17 sasa bado anacheza Ligi Kuu Tanzania Bara, tena kwa kiwango cha juu.
Ingawa umri unamtupa mkono na si kama Kaseja yule wa miaka ya 2000, lakini uwezo huu tu alionao, amewashinda makipa wengi vijana ambao kwa sasa walitakiwa wawe kama yeye alivyokuwa huko nyuma.
Pamoja na kusajiliwa kipindi cha dirisha dogo katikati ya msimu, lakini mechi chache tu alizocheza, bado amekuwa na uwezo mkubwa kuzuia michomo ya wachezaji wa timu pinzani, bado ni mwepesi kuruka, lakini pia hafungwi mabao ya kizembe.
Wengi walithibitisha hivyo kwenye mechi kati ya Kagera Sugar dhidi ya Simba.
Lakini tangu alipojiunga, ameifanya timu ya Kagera Sugar kuwa iliyofungwa mabao machache zaidi.
Ndiyo maana haikuwa ajabu alipochaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu wa mwezi Januari.
Kama makipa vijana wataendelea kuonyesha udhaifu wao, Kaseja huyo na ukongwe wake anaweza kugombaniwa na klabu kubwa, pia kucheza zaidi ya misimu mitatu mingine kwa kukosa changamoto kutoka kwa vijana.
2. Deogratius Munishi 'Dida'-Yanga
Ni mmoja kati ya makipa wazoefu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuzichezea klabu za Simba, Mtibwa Sugar, Azam FC na sasa Yanga. Ndiye kipa namba moja wa Yanga. Ni kipa aliyechangia kwa kiasi kikubwa Yanga kucheza mechi za kimataifa na kuwapo hapa ilipo katika Ligi Kuu na Kombe la FA.
Amekuwa akiiokoa timu yake kufungwa hata kwenye mechi ambazo mabeki wa timu hiyo wanakatika au hawako vizuri siku hiyo.
Ni mmoja kati ya makipa waliofanya vizuri sana msimu huu.
3. Aishi Manula-Azam
Bado anaendelea kuwa mmoja wa makipa bora vijana kwenye soka la Tanzania.
Wakati Kaseja na Dida wanaelekea ukingoni, Manula anabaki kuwa hana mshindani wa kweli wa kumpa presha kwenye eneo lake hilo, hasa kwa makipa wazawa.
Ameendelea kuwa na ubora ule ule, huku akilinda nafasi yake ya kuwa kipa namba moja wa timu ya Taifa, Taifa Stars.
Pamoja na timu yake ya Azam msimu huu kutokufanya vizuri kwenye Ligi Kuu hasa mzunguko wa kwanza, lakini bado ameendelea kuwa imara kwa kuokoa michomo ya wapinzani kwa ustadi mkubwa.
4. Daniel Agyei-Simba
Angalau wanachama na mashabiki wa Simba wamekuwa watulivu mara baada ya kusajiliwa kwa kipa Mghana Daniel Agyei kwenye kipindi cha dirisha dogo.
Ni baada ya kutokuwa na imani na Vicent Angban ambaye walidai alikuwa akifungwa mabao mepesi mno.
Agyei, ameonekana kutibu tatizo hilo, ingawa kwenye mechi za karibuni amekuwa akitatizwa na kukosekana na beki Methold Mwanjale, hivyo kuruhusu nyavu zake kutingishwa, kutokana na uzembe na makosa ya mabeki wake.
Alishawahi kucheza mechi zaidi ya sita bila kuruhusu bao, wakati beki ikiwa imara chini ya Mzimbabwe Mwanjale.
Anahesabika kuwa mmoja wa makipa waliotamba msimu huu.
5.Youthe Rostand-African Lyon
Moja ya vitu ambavyo African Lyon inajivunia ni kuwa na kipa mwenye uwezo wa hali ya juu kama Youthe Rostand.
Kipa huyo raia wa Cameroon alikuwa mwiba kwa washambuliaji anaposimama langoni kwa kuokoa makombora makali, huku akiwa na staili yake ya kupoteza muda timu yake inapokuwa mbele kwa ushindi.
Urefu wake, mwili uliojengeka, umekuwa ukiongeza ugumu kufungika.
Yeyote anayemfunga ni lazima awe amefanya kazi ya ziada na si kumfunga mabao rahisi na ya kizembe.
Kabla haijaangukia kwa Agyei, Simba ilikuwa na mpango wa kumsajili kipindi cha dirisha dogo.
Lakini pia kuna taarifa kuwa Yanga huenda ikamsajili kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Hakika ni kipa aliyefanya vizuri sana kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu inayoelekea ukingoni.