Licha ya kuwa matumaini waliyokuwa nayo ya kutinga nusu fainali ya michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17) na hatimaye kushiriki kombe la dunia kufutiliwa mbali baada ya kukubali kipigo toka kwa Niger, baadhi ya wachezaji wa Serengeti Boys wameaza kuitwa kufanya majaribio Ulaya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeeleza kuwa klabu kadhaa barani Ulaya zimevutiwa na vijana hao waliokuwa wamepangwa kundi B pamoja na Mali, Niger na Angola.
Afisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alithibitisha jana timu kadhaa za Ulaya zipo tayari kuwasaini makinda hao wanaochipukia katika soka.
“Wachezaji watatu ambao wapo Gabon na Serengeti Boys katika michuano ya Afrika kwa vijana (AFCON U17) watafanya majaribio nchini Uhispania, Ufaransa na Ubelgiji mwezi ujao,” alisema.
Lucas alisema wachezaji hao ni, Enrick Nkosi, Ally Msengi na Ally Ng’azi lakini hakutaja klabu ambazo zimewataka makinda hawa kutoka Tanzania.
Lucas alisema kuwa dili hilo lilifanywa na Mtanzania Abdallah Kondo ambaye ni wakala wa mshambuliaji wa Serengeti Boys, Yohana Mkomola.
Mkomola anatarajiwa kwenda Tunisia mwezi ujao kufanya majaribio katika klabu ya Etoile du Sahel ambayo ni miongoni mwa klabu kubwa Kaskazini mwa Afrika.
Msemaji huyo wa TFF alisema kwamba mipango yote ikienda sawa, watatangaza vilabu hivyo.