Kwa hakika ligi kuu Tanzania bara imefika patamu sana, kuna vita kuu mbili zinapiganwa kwa wakati mmoja na vita hizi ndizo zinafanya ligi kuwa na msisimko wa aina yake.
Vita ya kuwania ubingwa inayopiganwa na Simba na Yanga wakati vita nyingine ikipiganwa na timu za chini zinazokwepa kushuka dara na kuungana na JKT Ruvu ambayo tayari imeshatoa mkono wa kwaheri kwenye ligi kuu baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Toto Africans.
Leo Jumapili Mei 7, 2017 kutakuwa na vita ya aina yake pale kwenye uwanja wa taifa ambapo Simba itakuwa mwenyeji wa African Lyon. Mechi hii inahusisha vita mbili kwa wakati mmoja, vita ya kwanza ni ya ubingwa vs kukwepa kushuka daraja na nyingine ni ya kisasi vs ubabe.
Kama una kumbukumbu nzuri basi utakuwa unakumbuka kwamba, African Lyon ndio timu ya kwanza kuifunga Simba msimu huu 2016-2017 pale kwenye uwanja wa Uhuru walipoikalisha kwa bao 1-0 November 11, 2016.
Kisasi
Mechi ya leo Simba wataingia kwa kushambulia mwanzo mwisho huku ikiongozwa na wachezaji wake wa sehemu ya kiungo ambapo hata ukitazama wafungaji wengi wa magoli ya Simba wamekuwa ni wachezaji kutoka eneo la kiungo (Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin, Mohamed Ibrahim). Simba watataka kulipa kisasi kwa African Lyon baada ya kuwa timu ya kwanza kuipoka Simba pointi zote tatu kwenye mchezo mmoja.
Ushindi wa Yanga
Yanga ni mpinzani wa Simba katika ubingwa wa msimu huu, ushindi wa Yanga dhidi ya Tanzania Prisons unaifanya Simba leo kushinda kwa namna yoyote ili kuendelea kujiweka katika mazingira ya kuwania ubingwa wa ligi. Simba wanajua fika kwamba, wakishinda mechi yao dhidi ya Lyon watarudi kuongoza ligi kwa tofauti ya pointi tatu, ushindi utawafanya wafikishe pointi 62 na kuiacha Yanga ikiwa na pointi 59 katika nafasi ya pili. Sare itawarudisha pia katika nafasi ya kwanza lakini itakuwa ni kwa tofauti ya pointi moja huku Yanga wakiwa na faina ya mechi mkononi.
Siku zote Yanga huwa inaishukuma Simba na Simba inaisukuma Yanga kama ilivyo kwa wapinzani wa soka duniani Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.
Lyon hawapo eneo salama
African Lyon wapo nafasi ya 11 wakiwa na pointi 31 baada ya kucheza mechi 27, eneo ambalo si salama kwa hiyo wapo kwenye hatari ya kushuka daraja ikiwa timu za chini yao zitafanya vizuri halafu wao watavurunda katika mechi za mwisho.
Mechi hii ni muhimu kwa timu zote mbili Simba na African Lyon, Simba wanahitaji ushindi ili kuendelea kuweka hai matumaini yao ya ubingwa wa VPL msimu huu taji ambalo wamelikosa kwa misimu minne mfululizo. Ushindi kwa Lyon utakuwa na maana kubwa kwao kwa sababu bado hawajafikisha pointi 35 ambazo zinawafanya kujihakikishia kubaki ligi kuu kwa hiyo ni mechi muhimu kwao kushinda ukizingatia mechi zimebaki chache huku wakiwa kwenye nafasi ya hatari ya kushuka daraja.