Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema Serikali inatarajia kuandaa sheria itakayowabana madalali katika sekta ya ardhi.
Amesema lengo la sheria hiyo ni kuwabana madalali hao ambao wamekuwa wakiuza ardhi katika siku za mapumziko kutokana na sababu wanazozijua wao.
Lukuvi aliyasema hayo bungeni jana alipokuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18.
“Wizara hii itatunga sheria ya kuwadhibiti madalali wanaowaonea wananchi kwa kuuza nyumba siku za sikukuu na weekend. Hao kiama chao kinakuja kwa sababu tutawatungia sheria na tutawatambua kwa sifa zao kisheria.
“Hata wenye maeneo makubwa mijini, lazima tutaanza kuwatambua na kuwatoza kodi hata kama hawajayapima.
“Utakuta mtu anamiliki ekari 30 mjini, zote hizo za nini, utafika wakati tutawazuia kuuza maeneo hayo kwa sababu wanaiibia Serikali,” alisema Lukuvi.
“Katika hilo, Serikali imejipanga kuhakikisha kila ardhi iliyopo nchini, inapimwa na kutumika kwa usawa na haki kama ilivyokusudiwa kwani kuna watu wanatakatisha fedha zao kupitia sekta ya ardhi,” alisema Lukuvi.
Kuhusu utoaji wa miliki za ardhi, alisema wizara yake itaendelea kushirikiana na halmashauri na sekta binafsi kuhakikisha kila ardhi inapimwa na kumilikishwa.
“Katika mwaka wa fedha 2016/17, wizara iliahidi kuandaa hatimiliki za ardhi 400,000 na kutoa hati za hakimiliki za kimila 57,000.
“Hadi kufikia Mei 15 mwaka huu, wizara imetoa hatimiliki za ardhi 33,979 na imeratibu uandaaji wa hati za hakimiliki za kimila 35,002 na pia wizara imeandaa vyeti vya ardhi za viijiji 505.
“Lakini, katika mwaka wa fedha 2017/18, wizara yangu kwa kushirikiana na halmashauri nchini, itaandaa hatimiliki za ardhi 400,000, vyeti vya ardhi ya vijiji 1,000 na kutoa hati za hakimiliki za kimila 57,000.
“Ili kuwawezesha wananchi wengi kupata hatimiliki za ardhi, wizara inakusudia kupunguza tozo ya mbele ambayo hutozwa wakati wa kumilikisha kutoka asiliia 7.5 mpaka asilimia 2.5 ya thamani ya ardhi.
“Kwa hiyo, natoa wito kwa halmashauri zote nchini, kuhakikisha zinamilikisha viwanja vyote vilivyopimwa na kuandaa hati ili wananchi waweze kuwa na miliki salama,” alisema Lukuvi.
Wakati huo huo, alisema wizara yake itaendelea kuhakiki viwanja na mashamba nchini ili kubaini ukiukwaji wa masharti ya umiliki .
Pamoja na hayo, alisema baada ya kufanya uhakiki siku zilizopita, wizara yake imeshabatilisha miliki za viwanja 227 na mashamba 17 kutokana na ukiukwaji wa masharti. Viwanja na mashamba hayo, viko katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Iringa, Kagera na Morogoro.
Naye Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alimtaka Waziri Lukuvi atakapoanza kuchukua hatua kwa waliokiuka sheria za ardhi, asiangalie itikadi za kisiasa na badala yake kila mmoja achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
Kuhusu mradi wa viwanja 20, 000 jijini Dar es Salaam, aliitaka Serikali ifanye uhakiki wa viwanja hivyo ili kujua uhalali wa viwanja hivyo.
Pia, alitaka sheria za kimila za umiliki wa ardhi zinazowakandamiza wanawake, alitaka ziangaliwe upya ili wanawake nao wawe na haki ya kumiliki ardhi kama walivyo wanaume.
Naye Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka (CCM), alitaka migogoro ya ardhi inayohusisha wananchi na maeneo ya jeshi, itatuliwe haraka ili wananchi waishi kwa amani.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma (CUF), alilalamikia bei ya nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kusema zinauzwa kwa bei kubwa ingawa viongozi wa shirika hilo wamekuwa wakisema zinauzwa kwa bei ndogo.