Rais John Magufuli ametangaza kuwa Serikali yake itatoa nyongeza ya mshahara ya mwaka na kupandisha madaraja ya kazi kuanzia Bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2017/18.
Aidha, amepiga marufuku wafanyakazi wa Serikali kuhamishwa kituo cha kazi bila kulipwa stahiki zake, akisema lengo la hatua hiyo ni kuepusha madai yasiyo na sababu.
Rais Magufuli alisema hayo jana kwenye sherehe za Sikukuu ya Mei Mosi zilizofanyika kitaifa Moshi mkoani Kilimanjaro.
Alisema Serikali ililazimika kufanya ukaguzi wa watumishi wake wote kabla ya kufanya uamuzi wowote kuhusu maslahi ya wafanyakazi na kwamba baada ya kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti vya kughushi atakaa na Baraza la Mawaziri kufanya maboresho.
“Acheni tufagie nyumba kwanza, mlitaka nitangaze nyongeza huku wakiwamo watumishi hewa na wasio na vyeti? … Mwaka huu tutapandisha madaraja ya kazi na kuweka nyongeza ya mishahara kuwa sawa na madaraja stahiki ambayo yapo kisheria,” alisema.
Rais alisema mchakato wa kusafisha watumishi wenye upungufu na hewa ulikuwa mgumu, hivyo ni wakati mwafaka kwa ambao wanastahiki kupata promosheni kunufaika, kwani wangefanya kabla kundi la wafanyakazi 19,000 waliondolewa lingekuwapo.
Magufuli alisema pamoja na kuongeza mishahara na kupandisha vyeo, Serikali inatarajia kuajiri zaidi ya wafanyakazi 52,000 ili kuziba mapengo mbalimbali katika utumishi wa umma.
“Mei Mosi si kwa ajili ya Tanzania bali duniani kote. Ni siku ya kukumbushana na kutafakari mambo kuhusu wafanyakazi na kutatua matatizo yanayowakabili, hivyo nimechukua changamoto zenu na ninaahidi kuzifanyia kazi,” alisema.
Alipongeza viongozi wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), kwa kutambua dhamira ya Serikali, hivyo kuwaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano ili kuchangia maendeleo ya Taifa.
Aidha, alisema changamoto za kisheria zinazowakabili wafanyakazi, waziri husika atazifikisha bungeni na zikipitishwa atasaini muda huo huo.
“Nawahakikishia kuwa tunaanza ukurasa mpya. Ndiyo maana mnaona hii siku ni tofauti. Serikali tumeamua kuimarisha maslahi ya wafanyakazi. Na nyie muwe tayari kuchapa kazi,” alisema.
Rais Magufuli alisema wafanyakazi ndio injini ya maendeleo katika Taifa lolote kubwa duniani, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja kwa maslahi ya nchi na wananchi.
Kuhusu fao la kazi, alisema Serikali inalifanyia kazi na kuna mchakato unaendelea mfanyakazi anapoacha ajira kabla ya kustaafu, alipwe sehemu ya mafao.
Akizungumzia bima, alisema Serikali inaendelea na utaratibu wa kuanzisha fao la Bima ya Ajira na wadau wameshatoa maoni, hivyo wakati ukifika watapewa taarifa rasmi.
Akijibu hoja ya uhuru wa wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi, alisema suala hilo lilishazungumzwa mwaka jana na lipo kwa mujibu wa sheria na hakuna mwajiri aliye juu ya sheria.
Kwa upande mwingine, Rais Magufuli ameziagiza wizara na taasisi kuunda mabaraza ya wafanyakazi kulingana na mahitaji na kuwa kwa sasa yapo mabaraza 478.
Aidha, alitaka waajiri kutoa mikataba ya ajira kwani ni jambo la kisheria na si hiari.
Akijibu madai ya wafanyakazi baada ya kuhamishwa eneo la kazi, Rais aliwataka wafanyakazi kutohama eneo bila kulipwa stahiki zao, kwani ni kinyume na sheria.
Rais Magufuli alisema hakuna sababu ya mfanyakazi kuhamishwa bila kulipwa, kwani kinachoendelea ni lawama kwa Serikali, jambo ambalo hataki kulisikia tena.
Aidha, kuhusu mfumuko wa bei, Rais alisema Serikali ipo kwenye mkakati wa kuhakikisha hali hiyo inadhibitika, huku akibainisha kuwa mvua zinazoendelea kunyesha zitafanikisha mchakato huo.
Halikadhalika Rais alisisitiza kuwa Serikali ina mpango wa kuboresha na kufufua viwanda hali ambayo itachangia kuongezeka kwa ajira.
Alisema kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii jumla ya dola za Marekani milioni 156 zitatumika kujenga viwanda nchini.