Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga mheshimiwa Azza Hilal Hamad kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ametoa msaada wa vifaa tiba ikiwemo vitanda vya kisasa vya kujifungulia,vitanda vya wagonjwa na viti vya wagonjwa katika vituo vya afya na zahanati katika halmashauri ya Shinyanga vijijini na Kishapu vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 33.
Mbunge huyo amekabidhi vifaa tiba hivyo katika Kituo cha afya Tinde,zahanati ya Solwa,zahanati ya Nyashimbi,kituo cha afya Samuye katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga vijijini na kwa upande wa Kishapu ni Kituo cha afya Nhobola,Mwang’haranga,Dulusi na Songwa.
Vifaa hivyo vinatokana na jitihada zilizofanywa na mbunge huyo Azza Hilal Hamad kufika katika ubalozi wa China nchini Tanzania kuomba asaidiwe vifaa tiba hivyo ili kukabiliana na vifo vya mama na mtoto mkoani Shinyanga.
Akizungumza jana Jumamosi Mei 13 wakati wa kukabidhi vitanda vitatu vya kisasa vya kujifungulia,vitanda 9 vya wagonjwa na viti vitatu (wheel chairs) vyenye thamani ya shilingi milioni 9.7 katika kituo cha afya Tinde kilichopo Shinyanga vijijini,mheshimiwa Hamad alisema vitasaidia kupunguza adha ya upungufu wa vitanda katika kituo hicho kilichojengwa mwaka 1920.
“Kituo cha afya Tinde kinahudumia tarafa yote ya Itwangi na kata za jirani,kilikuwa na upungufu wa vitanda 28,leo nimeleta vitanda hivi kusaidia wananchi wapate huduma bora,naomba wananchi muwe mstari wa mbele kuunga mkono shughuli za maendeleo,ni aibu kuona kituo hiki kilichojengwa kabla ya uhuru kikiwa hakina majengo ya kutosha ikiwemo nyumba za watumishi na wodi kwa ajili ya wagonjwa”, alieleza Hamad.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga mheshimiwa Azza Hilal Hamad kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) akipokelewa kwa shangwe katika kituo cha afya Tinde kilichopo Shinyanga vijijini alipofika kukabidhi vitanda vya kisasa na viti vya wagonjwa vyenye thamani ya shilingi milioni 9.7
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga mheshimiwa Azza Hilal Hamad kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwahutubia wakazi wa kata ya Tinde wakati akikabidhi vifaa tiba hivyo.
Viti vya wagonjwa,vitanda vya kujifungulia kwa akina mama na vitanda vya kulalia wagonjwa vilivyotolewa na mbunge Azza Hilal kwa ufadhili wa ubalozi wa China nchini Tanzania.