Mwamuzi mtanzania Frank John Komba ni miongoni mwa waamuzi walioorodheshwa kuchezesha michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 (U-17 Africa Cup of Nations) michuano ambayo imepangwa kufanyika Gabon.
Komba yupo kwenye orodha ya waamuzi wasaidi (Assistant Referees au washika kibendera) na ni mwamuzi pekee kutoka Tanzania aliyepata fursa hiyo kutoka Tanzania. Komba anaungana na waamuzi wengine wawili kutoka ukanda wa Afrika Mashariki Pacifique Ndabihawenimana (mwamuzi wa kati kutoka Burundi na Davies Ogenche Omweno (mwamuzi wa kati kutoka Kenya).
Hii ni habari njema kwa soka la Tanzania ambapo wadau wamekuwa wakipaza sauti zao kutaka wachezaji wa Tanzania kujituma ili kupata fursa ya kucheza nje lakini pia wamekuwa wakihoji kwa nini makocha wengi wazawa hawapati nafasi za kufundisha timu nje ya nchi hali kadhalika kwa waamuzi wa nyumbani wamekuwa hawapati mechi za kutosha za kimataifa licha ya kuwa na beji za FIFA.
Timu ya taifa ya vijana ya Tanzania ‘Serengeti Boys’ ni miongoni mwa timu ambazo zitashiriki michuano hiyo ambayo inatarajia kuanza May 14 mwaka huu.
Shaffihdauda.co.tz inampongeza Frank John Komba kwa kuteuliwa kuwa miongoni mwa waamuzi watakaochezesha michuano ya vijana Afrika na kumtakia kila la heri ili afanye vizuri na kusonga mbele.